Friday , 29 September 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Mbowe awafunda viongozi Chadema
Habari za SiasaTangulizi

Mbowe awafunda viongozi Chadema

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema Taifa
Spread the love

SAA chache baada ya Dkt. Vincent Mashinji, Katibu  Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na wenzake kukamatwa na Polisi kwa mahojiano wilayani Mbamba Bay, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa ameibuka na kueleza haya, anaandika Mwandishi wetu.

Kuwa kiongozi wa upinzani awe Mbunge, Diwani, au Mwenyekiti wa Mtaa, kunahitaji roho ngumu na kwamba hiyo si kazi ya watu wenye kupenda fedha, bali ni ya maumivu, kudhalilishwa, kunyimwa ushirikiano, kufungwa wakati wowote na kunahitaji msimamo wa hali ya juu.

“Upinzani ni wito, wenye roho nyepesi hawawezi, kama ningekuwa napenda fedha, nina roho nyepesi, ningeshachukua hizo pesa na ningeshakimbia kabisa.

“Wanaowania nafasi za uongozi na viongozi wa Chadema wanahitaji kuwa na msimamo wa hali ya juu.

“Mara nyingi wanaowania nafasi kwa upande wa upinzani, ni wale waliokomaa, lakini katika uchaguzi uliopita, chama kilichopata watu wengi ni Chadema. Kutokana na mfumo huo wa kuwafungulia milango, wakaingia wengi, mbu, mende na mambo mengine.

“Kuondoka kwa madiwani wa Chadema kunasababishwa na baadhi ya watendaji wa Serikali hasa wakuu wa wilaya ambao wanataka kumfurahisha Rais.

“Inashangaza kuona wote wanaojiuzulu wanatoa kauli moja ya kumsifu Magufuli, ina maana hawana sababu nyingine labda pengine Chadema kuna matatizo, sera zao mbovu, kuna hiki na hiki hakijakaa sawa.

“Juhudi za kuwarubuni viongozi wa Chadema zipo katika majimbo yote ya Chadema na juhudi hizo zinapata nguvu zaidi mahali ambako kuna mkuu wa wilaya dhaifu ambaye anatumia nguvu za ziada.

“Tumebaini kuwa baadhi ya wakuu wa wilaya ndiyo wanaotumiwa na wamewekwa kwa makusudi kwa ajili ya kuua upinzani nchini.

“DC anawahimiza wanachama na viongozi eti wapeleke barua za kujizulu kwake, kwa sababu ana jeuri ya mamlaka. Kisheria hana mamlaka ya kupokea barua ya kujiuzulu kwa mwanasiasa, tumebaini hawa baadhi ya watendaji wanatumiwa na kuahidiwa makubwa endapo watawadhibiti wapinzani.

“Tulipata tetesi za kujiuzulu kwa madiwani lakini hatukutaka kuchukua uamuzi wa kuwafukuza kwani si vizuri kuishi kwa tetesi lakini kwa kuwa wameamua kuondoka nawatakia kila heri.

“Baadhi ya madiwani hao walionekana kwenye vikao vya CCM mtu anayezidiwa akili na kudanganywa kwa fedha hata akibaki katika chama hatakuwa na maana.

“Kuliko kubaki na watu wengi wanaopenda fedha, wanaohadaiwa kwa rushwa, bora tubaki watu wachache wenye maadili.

“Licha ya Serikali kuudhofisha upinzani, sisi kama chama tunaamini kuwa safari hii ni kama ya treni ya kwenda Kigoma ambayo wapo wanaopanda na wanaoshuka.

“Bado tunavuna maelfu ya wana CCM, alianza Edwin Mtei, lakini sasa tunazungumzia wanachama zaidi ya milioni sita, Muelewe kuwa upinzani haudhoofiki, bali unakua.

“Wale waliodhani watapata ulaji kama wa fedha, ndiyo wanaokuwa wepesi kuondoka na kwenda kutafuta wanachokitaka.

“Tuna imani watabaki wachache wenye imani na nafasi za walioondoka zitachukuliwa na wengine walio bora zaidi.

“Kuhusu kuswekwa rumande kwa saa 48 kwa amri za wakuu wa wilaya, Kuna utaratibu wa kufanya. DC sio polisi, anaweza kuagiza polisi, kamkamateni fulani kisha mumhoji na kisha afunguliwe mashtaka, lakini si kumuweka ndani kwa saa 48. Haya maagizo yote yanatolewa na ngazi za juu. Sisi sasa tunawashtaki hao Ma-DC wote na hata mimi nimemshtaki DC wa Hai, kwa kuharibu miradi yangu”.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Serikali yawaangukia viongozi wa dini

Spread the loveSERIKALI imewaomba viongozi wa dini, waendelee kuelimisha wananchi kudumisha amani...

Habari MchanganyikoTangulizi

Afya ya akili yatajwa chanzo kuvunjika ndoa

Spread the loveCHANGAMOTO ya afya ya akili, imetajwa kuwa chanzo cha migogoro...

Habari za Siasa

Azzim Dewji aitaka Serikali iwanyooshe mafisadi

Spread the loveMFANYABIASHARA maarufu nchini, Azzim Dewji, ameitaka Serikali iwachukulie hatua wezi...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Kapinga: Usambazaji umeme vijijini mwisho Desemba 2023

Spread the love  NAIBU Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, amesema ifikapo mwezi...

error: Content is protected !!