September 23, 2021

Uhuru hauna Mipaka

ACT-Wazalendo wamkunjulia makucha Rais Samia

Spread the love

 

CHAMA cha siasa cha upinzani nchini Tanzania-ACT Wazalendo, kimesikitishwa na kauli ya Rais wa Taifa hilo, Samia Suluhu Hassan kuwa mikutano ya hadhara pamoja na Katiba mpya vinapaswa kusubiri. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

ACT-Wazalendo, kimetoa wito kwa Rais Samia kutafakari upya msimamo huo kwani kuendelea kusimamia uamuzi huo “atakuwa ameutia doa kubwa utawala wake na kupanda mbegu itakayolirudisha nyuma na kuligawa Taifa.”

Hayo wameyasema leo Jumanne, tarehe 29 Juni 2021 na chama hicho ikiwa ni siku moja imepita tangu Rais Samia aseme, masuala hayo ni muhimu kwa nchi, lakini yanapaswa kusubiri kwanza asimamishe uchumi wa nchi.

Rais Samia, alitoa kauli hiyo jana Jumatatu, Ikulu ya Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na wahariri na waandishi wa vyombo vya habari, kuhusu siku 100 za utawala wake.

Aliingia madarakani tarehe 19 Machi 2021, kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais John Pombe Magufuli, kilichotokea 17 Machi 2021, Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam.

Rais wa Tanzania,
Samia Suluhu Hassa

Taarifa ya Janeth Rithe, Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma, ACT Wazalendo imesema, chama hicho kinaamini Katiba ni msingi na kichocheo cha maendeleo.

“Hakuna maendeleo ya uhakika yanayoweza kupatikana bila kwanza kuweka msingi madhubuti wa Kikatiba.”

“CCM ambayo imekuwepo madarakani tangu uhuru haiwezi kuwakosesha wananchi haki yao ya kupata Katiba mpya kwa kisingizio cha kujenga uchumi wa nchi,” imeeleza taarifa hiyo

Kuhusu mikutano ya hadhara, ACT-Wazalendo imesema, hiyo ni haki inayolindwa na Katiba na Sheria. Katiba ya Tanzania (Ibara ya 3) na Sheria ya Vyama vya Siasa (Kifungu cha 11) vinatoa haki ya Vyama vya Siasa kukusanyika.

“Rais wa nchi ambaye ameapa kuilinda na kuitetea Katiba na sheria za nchi hapaswi kuzuia haki ambayo imetolewa na kulindwa na Sheri.”

Chama hicho kimetoa wito kwa “Rais Samia Suluhu atafakari upya msimamo wake kuhusu Katiba mpya na haki ya vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara.”

“Iwapo ataendelea na msimamo huo, bila shaka, atakuwa ameutia doa kubwa utawala wake na kupanda mbegu itakayolirudisha nyuma na kuligawa Taifa.”

Rais Samia alisema, mikutano ya hadhara kwa sasa ifanyike ya ndani tu au madiwani na wabunge wafanye kwenye maeneo yao.

error: Content is protected !!