Thursday , 9 May 2024
Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Hakuna fedha za Rais

Spread the love

KUNA mambo machache mazuri ya kujifunza kutoka kwa Margaret Thatcher, waziri mkuu wa Uingereza kuanzia mwaka 1979 hadi 1990.

Baada ya kusumbuliwa na kauli kama “serikali ina fedha” au “fedha za umma”, mama huyo aliyebatizwa jina la Irony Lady, tarehe 14 Oktoba 1983 aliitisha kongamano la chama  chake cha Wahafidhina (Conservatives), akapasua ukweli.

Somo alilowapa Wahafidhina linafaa wapewe “chawa wa mama” ambao wameugua ugonjwa wa upotoshaji kuhusu vyanzo vya fedha za miradi ya maendeleo.

Thatcher aliwaambia, “Tusisahau kamwe ukweli huu wa kimsingi: Serikali haina chanzo chake cha fedha isipokuwa fedha ambazo wananchi hujipatia wenyewe. Iwapo Serikali itapenda kutumia zaidi inaweza kufanya hivyo tu kwa kukopa akiba yao au kwa kukutoza kodi zaidi. Siyo vizuri kufikiri kwamba mtu mwingine atalipa – huyo ‘mtu mwingine’ ni wewe. Hakuna kitu kinachoitwa fedha za umma; fedha ni za walipakodi tu”.

Imeeleweka? Miaka michache iliyopita alikuwepo rais wa awamu ya tano, John Magufuli ambaye katika hotuba zake alikuwa akiwaambia Watanzania, kwamba kama nchi, “tuna fedha za kutosha kugharimia miradi mingi mikubwa ya maendeleo”. Magufuli akaweka mkazo katika ukusanyaji kodi na udhibiti wa matumizi.

Magufuli hakuleta kitu kipya, bali aliendeleza walichoanzisha watangulizi wake. Ni Mwalimu Julius Nyerere aliyewaambia Watanzania kwamba “hatuna mjomba wa kutupatia fedha.”

Katika kuhakikisha nchi inaondokana na ugonjwa wa “ruksa” ambapo hata kutolipa kodi ilikuwa ruksa katika awamu ya pili, Benjamin Mkapa aliunda taasisi kadhaa – Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kupambana na Rushwa (Takuru sasa Takukuru).

Rais Samia Suluhu Hassan

Jakaya Kikwete aliendeleza katika awamu yake, lakini Magufuli alisimamia ukusanyaji mapato huku “akikataa misaada na mikopo” aliyodai ina masharti yasiyotekelezeka. Wafanyabiashara walibanwa, wakwepa kodi walitikiswa, na njia nyingine zisizorafiki zilitumika kupata fedha kutoka kwa wananchi.

Japokuwa,  fedha za miradi mikubwa kama ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), ujenzi wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere, ujenzi wa vituo vya mabasi na mengineyo zilitokana na mikopo yenye riba kubwa kutoka mabenki ya kigeni, ukweli utabaki serikali italipa mikopo hiyo kutokana na kodi za wananchi.

Serikali inakamua kodi, inakusanya ushuru sijui maduhuli na kupokea gawio, lakini fedha hizo zikitoka TRA inayokusanya na kuingia Wizara ya Fedha kwa ajili ya kugharimia miradi ya maendeleo zinabadilika na kuwa fedha za rais. Vipi?

Hivyo chawa wa mama wanaodai “Tunampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea fedha za kujenga barabara, shule, kuchimba visima; mama anatupenda sana” ni propaganda za kitoto. Thatcher, Magufuli, Kikwete na Mkapa wanasema fedha zinazokwenda kwenye miradi ya maendeleo zinatokana na kodi za wananchi, hizi za mama zinatoka wapi?

Thatcher aliwaambia Wahafidhina hakuna fedha za umma; Mkapa alisema fedha ni kodi za wananchi; wasomi chawa wa mama wanadai fedha ni za rais. Ebo! CCM kubalini ukweli mchungu: Hakuna fedha za Rais, bali ni za wananchi walipakodi. Makala hii imeandikwa na Joster Mwangulumbi. Anapatikana kwa simu namba 0753626751

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Rais Samia: Matumizi ya nishati safi sio anasa, ladha ipo

Spread the loveRAIS Samia Suluhu Hassan amesema matumizi ya nishati safi kwa...

Habari za SiasaTangulizi

Samia: Kuanzia Agosti marufuku kutumia mkaa, kuni

Spread the loveRAIS Samia Suluhu Hassan amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya...

Habari za SiasaTangulizi

Mwendokasi Kigogo – Segerea kujengwa awamu ya 5

Spread the loveNaibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Festo Dugange...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Rais Samia ni Mzanzibari: Shida Iko Wapi?

Spread the loveTAIFA linakabiliwa na upungufu wa fikra sahihi. Upungufu huu unaonekana...

error: Content is protected !!