Tuesday , 30 April 2024
Home Habari Mchanganyiko CCBRT yaita watoto wenye mguu kifundo
Habari Mchanganyiko

CCBRT yaita watoto wenye mguu kifundo

Brenda Msangi, Mkurugenzi wa Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya CCBRT
Spread the love

 

HOSPITALI ya CCBRT, imetoa wito kwa wazazi wanaojifungua watoto wenye tatizo la mguu kifundo, kuwafikisha hospitali mapema kwa ajili ya kupatiwa matibabu. Anaripoti Jemima Samwel DMC … (endelea).

Wito huo umetolewa leo Alhamisi, tarehe 3 Juni 2021 na Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa CCBRT, Brenda Msangi, akizungumzia maadhimisho ya siku ya kimataifa ya Mguu Kifundo, jijini Dar es Salaam.

“Watoto kuletwa hospitalini wakiwa zaidi ya mwaka mmoja, ni vibaya. Jambo ambalo hufanya matibabu yake kuwa magumu kutokana na kukomaa kwa viungo. Inashauriwa kuanza matibabu ya ulemavu huu, wiki mbili baada ya mtoto kuzaliwa,” amesema Msangi.

Akizungumzia hali ya tatizo hilo nchini, Msangi amesema bado kuna changamoto mbalimbali zinazosababisha watoto wenye mguu kifundo kubaki na ulemavu, ikiwemo wazazi au walezi wao kutofuatilia matibabu.

Pamoja na kushindwa kumudu gharama za usafiri wa kwenda hospitali, hasa wale wanaotoka maeneo ya vijijini.

“Kujirudia kwa ulemavu kunatokana na uelewa mdogo wa wazazi na walezi wa watoto wenye shida hiyo. Pia umbali kutoka nyumbani kwenda hospitali na hali ngumu ya uchumi, hupelekea kukatisha matibabu kwa kushindwa kuhudhuria kliniki kwa tarehe pangwa,” amesema Msangi.

Msangi amesema mwitikio wa wazazi kuwapeleka watoto hospitalini ni mdogo, na kutoa wito kwa jamii kuanza kuwapeleka mapema ili waepukane na ulemavu wa kudumu.

“Idadi bado ni ndogo ikilinganishwa na ukubwa wa tatizo, kwani watoto wengi hubakia katika jamii zetu wakiishi na ulemavu huu unaotibika. Na hivyo kuwakosesha fursa mbalimbali katika kukabiliana na changamoto za maisha,” amesema Msangi.

Mguu wenye kifundo ukinyoshwa na kufungwa POP

Kuhusu maadhimisho ya siku ya Mguu Kifundo duniani, inayoadhimisha tarehe 3 Juni kila mwaka, Msangi amesema, imeanzishwa ili kumuenzi Dk. Ignacio Ponseti, aliyegundua namna ya kutibu tatizo hilo.

“Tarehe hii ilitengwa mahsusi ili kuitambua siku ya kuzaliwa kwa Dk. Ponseti (1914-2009), aliyegundua matibabu ya mguu kifundo kwa kutumia njia ya Ponseti,” amesema Msangi.

Msangi amesema, CCBRT ilianza kutoa matibabu ya mguu kifundo 2001 na ilipofika 2008, ilianza kutumia njia ya Ponseti .

“Hospitali ya CCBRT ilianza kutoa matibabu ya mguu kifundo mwaka 2001 na ilipofika mwaka 2008, tulianza rasmi kutoa matibabu ya ulemavu huu kwa kutumia njia ya Ponseti, njia nyepesi na madhubuti katika kurekebisha ulemavu huo,” amesema Msangi.

Msangi amesema, mguu kifundo hutokea kwa mtoto mmoja kati ya watoto 750, wanaozaliwa hai kila mwaka, ambapo zaidi ya 800,000, huzaliwa na mguu kifundo kila mwaka ulimwenguni kote na kwamba kati ya hao, asilimia 80 huzaliwa katika nchi zinazoendelea.

Amesema nchini Tanzania, takwimu zinaonyesha watoto 2,200 hadi 3,000, huzaliwa na mguu kifundo kila mwaka.

“CCBRT imeendelea kuwa mtoaji mkubwa wa matibabu ya ulemavu huu hapa nchini. Kwa mwaka huwaona watoto wapya wenye tatizo la mguu kifundo, takribani 400,” amesema Msangi.

Mguu kifundo ni aina ya ulemavu wa kuzaliwa nao, ambapo mtoto anaweza kuzaliwa huku nyayo moja au zote kujikunja kwa ndani na kwa kutazama chini.

Hali hiyo inaathiri mifupa , misuli, ngozi na mishipa ya damu ya mguu. Na inasemekana hili tatizo huathiri zaidi watoto wa kiume kuliko wa kike.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari Mchanganyiko

Oryx gesi yagawa mitungi, majiko 100 kwa waandishi wa habari Dar

Spread the loveKAMPUNI ya Oryx Gesi Tanzania imegawa mitungi 100 ya gesi...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mavunde ataja malengo “Vision 2030”

Spread the loveWAZIRI wa Madini amesema dhana ya “Vision 2030” inakusudia kuiendeleza...

Habari MchanganyikoMichezo

Wanamichezo Mei Mosi wachangia wahitaji vitu vya mil. 11.5

Spread the loveWanamichezo wanaoshiriki Michezo ya Mei Mosi Taifa 2024 jijini Arusha...

Habari Mchanganyiko

TMA yapongezwa kuimarisha ubora na usahihi wa taarifa za Hali ya Hewa

Spread the love  WAFANYAKAZI wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA),...

error: Content is protected !!