Thursday , 2 May 2024
Home Kitengo Maisha Afya Mbowe athibitisha mwanawe kupata Corona
AfyaHabari za SiasaTangulizi

Mbowe athibitisha mwanawe kupata Corona

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema
Spread the love

MWENYEKITI wa Chadema, Freeman Mbowe, amekiri kuwa mmoja wa watoto wake, Dudley Mbowe, amekutwa na ugonjwa wa Corona. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Katika taarifa yake kwa umma aliyoitoa leo jioni, tarehe 24 Machi 2020, Mbowe amesema, mtoto wake huyo, amethibitika kuwa na virusi vya Corona na sasa anapatiwa matibabu kwenye hospitali ya Mwananyamala, jijini Dar es Salaam. 

Anasema, “…ni kweli mwanangu Dudley amethibitika kupatikana na virusi vya Corona baada ya kupata homa za vipindi, kuumwa kichwa mfululizo na kukohoa kwa siku tano. 

“Mama yake, ambaye ni daktari alipobaini hali hiyo, alizitaarifu mamlaka za serikali zinazoshughulikia janga hili ambapo ziliagiza mhusika kufikishwa hospitali ya Mwananyamala kwenye vipimo zaidi ambapo amethibitika rasmi kuwa ana virusi vya Corona.”

Kukiri kwa Mbowe kuwa mmoja wa wanafanmilia yake amepatikana na Corona, kumekuja muda mfupi baada ya mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kuutangazia ulimwengu kuwa mtoto wa kwanza wa mwanasiasa huyo, ni miongoni mwa waliopatikana na virusi hivyo.

Akizungumza na mamia ya wananchi katika kituo kikuu cha mabasi cha Ubungo, leo asubuhi, Makonda alisema, hatua ya Mbowe kufuta mikutano ya hadhara aliyoitisha nchi mzima, imetokana na mwanawe kuugua ugonjwa huo.

Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Katika taarifa yake Mbowe amekiri kupata ushirikiano wa kutosha kutoka mamlaka za serikali, hasa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Ummy Mwalimu; Katibu Mkuu wa wizara hiyo, mganga mkuu wa serikali na wataalam wengine.

Akizungumzia hali ya kijana wake, Mbowe anasema, “Dudley anaendelea vizuri. Homa zimekwisha. Kichwa kimepona. Lakini bado anakohoa kiasi na yuko chini ya uangalizi maalum kwenye “isolation.”

Kwa mujibu wa Mbowe, kijana huyo ambaye anasimamia kampuni ya Free Media, hajasafiri nje ya nchi mwaka huu na hivyo, maambukizi yake atakuwa ameyapata mkoani Dar es Salaam.

“Ugonjwa huu haupaswi kuwa siri japo kuna miiko inayoongoza utaji wa taarifa za wagonjwa,” anaeleza Mbowe na kuongeza, “tatizo ni kubwa kuliko tulivyojiandaa na tunavyojiandaa.”

Mbowe ambaye ni mbunge wa Hai, mkoani Kilimanjaro na Kiongozi wa Kambi rasmi ya upinzani bungeni (KUB), ameeleza kuwa tangu Makonda kutoa madai hayo, watu wengi wamekuwa wakiitafuta familia yake kwa lengo la kutaka kujua ukweli na suala hilo.

“Pengine kupitia ushuhuda wangu, tutaweza kuokoa wengi katika nchi yetu. Hakika leo kila mmoja anastahili kujua janga hili liko mlangoni mwake! Nimekiri kupata ushirikiano “kwa kiwango kilichowezekana. 

“Sina uhakika ni wangapi watapata ‘bahati’ hiyo. Nimejifunza mengi. Nazungumza kwa mamlaka ya kuwa mhanga na shuhuda wa hali halisi tuliyo nayo,” ameeleza. 

Anasema, “tuna mlima mrefu wa kupanda. Hakika Serikali inahitaji msaada. Mlipuko hauko mbali. Tuelezane ukweli tusijechelewa. Njia mojawapo muhimu ya kulishinda tatizo ni kulikubali na kulikabili kwa nguvu zote na kwa umoja wetu.”

Kwa muda wa zaidi wa miezi mitatu sasa, ulimwengu umekubwa na sintofahamu ya virusi vya Corona mbako inaaminika maelfu ya watu wamekufa na wengine kadhaa kuugua ugonjwa huo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mavunde ataja malengo “Vision 2030”

Spread the loveWAZIRI wa Madini amesema dhana ya “Vision 2030” inakusudia kuiendeleza...

Habari za Siasa

Mavunde aomba bilioni 231.9 bajeti wizara ya madini

Spread the loveWAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde leo Jumanne amewasilisha hotuba ya...

Habari za SiasaTangulizi

Lissu amjibu Fatma Karume kuhusu Rais Samia

Spread the love  MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)...

Habari za SiasaTangulizi

Dk. Slaa: Watanzania iungeni mkono Chadema uchaguzi 2025

Spread the loveMWANASIASA mkongwe nchini Tanzania, Dk. Wilbroad Slaa, amewataka watanzania wakiunge...

error: Content is protected !!