Friday , 3 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mbowe, Zitto: Tulionya, tunaonya tena
Habari za SiasaTangulizi

Mbowe, Zitto: Tulionya, tunaonya tena

Spread the love

ZITTO Kabwe, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo ameonya mkakati wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kutenganisha wapiga kura visiwani Zanzibar. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Wakati Zitto akionya, Freeman Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema Taifa ametuhumu tume hiyo na ile ya Tanzania Bara (NEC) kwamba zinatumika vibaya.

Ni baada ya ZEC kueleza, kwamba inakusudia watumishi wake na vikosi vya usalama kupiga kura kabla ya siku moja ya uchaguzi.

“Nilionya wakati huo, naonya, tume isijiamulie na Wazanzibari hawatokubali kupora haki yao,” amesema Zitto alipoongea na chombo kimoja cha habari nchini.

ZEC imeeleza, dhamira ya kuweka utaratibu huo ni kutaka kuhakikisha watumishi hao wanatekeleza majukumu yao siku ya uchaguzi.

“Kura hiyo itawahusisha vikosi vya ulinzi na usalama na watendaji wa tume, ili watumishi hao watekeleze majukumu yao siku ya uchaguzi,” amesema Thabit Idarous, Mkurugenzi wa (ZEC) wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu uchaguzi mkuu wa mwakani visiwani humo.

Amefafanua, takwa hilo linaendana na marekebisho ya Sheria ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar Na. 4 ya Mwaka 2018 na kuwa, sheria hiyo inatoa nafasi kwa makundi hayo kupiga kura siku moja kabla.

Hata hivyo, Zitto amesema, mabadiliko hayo yaliyofanya na chama kimoja (CCM) kupitia Baraza la Wawakilishi Zanzibar, yalizingatia maslahi ya chama hicho.

“Kwanza mabadiliko yatazuia vyama kukagua uhalali wa kura, hayaambatani na daftari, tofauti la watu wa vikosi, hapatakuwa na mawakala wa vyama kwenye kambi za jeshi,” amesema na kuongeza;

“Uamuzi umefanywa na upande mmoja, na hatua walizochukua za kufanya mabadiliko ya sheria ni wa maslahi ya chama kimoja.”

Zitto ameeleza kwamba mazingira ya kisiasa kwa sasa visiwani Zanzibar ni ya kutoaminiana, akingeza “Mpaka sasa, hatutambui serikali na Baraza la Wawakilishi.”

Katika kurejesha imani kuelekea uchaguzi huo Zitto ameshauri kuwepo kwa majadiliano kwa pande zote na kufikia muafaka.

“Uchaguzi wa Zanzibar umekuwa na vurugu na kumwaga damu. Ni muhimu kutaka kuwa na mazingira ya kuwezesha uchaguzi uwe huru na haki,” amesema.

Mbowe amesema, kinachofanywa na ZEC ni kuandaa wapiga kura zaidi ya idadi halisi kwa ajili ya kupata ushindi “huku ni kuandaa ushindi kwa chama tawala,

“Itakuwa ni kuhalalisha wapige kura wengi ziada kwa ajili ya kupata ushindi kwa chama tawala tofauti na idadi halisi ya wapiga kura,” amesema Mbowe.

Kiongozi huyo wa upinzani na Mbunge wa Jimbo la Hai amesema, maandalizi hayo yanataka kuwaweka vikosi hivyo kubaki na kazi ya kuthibiti wapinzani siku ya kupiga kura.

“Tunahitaji tume huru ya uchaguzi ili haya mambo yafikiwe kwa maridhiano,” amesema.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Sabaya afutiwa kesi, ruksa kugombea uongozi

Spread the loveMwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali DPP leo Ijumaa amefuta rufaa...

Habari za Siasa

Serikali yasaka bilioni 3 kujenga daraja Mto Mpiji

Spread the loveSerikali imesema inaendelea na juhudi za kutafuta fedha kiasi cha...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema kwafukuta kisa chaguzi, Lissu aibua tuhuma nzito

Spread the loveCHAGUZI za kusaka viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo...

Habari MchanganyikoTangulizi

Kimbunga “HIDAYA” chaendelea kuimarika, wananchi wapewa tahadhari

Spread the loveMAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kutoa taarifa...

error: Content is protected !!