Thursday , 9 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Matumizi mabaya ya fedha yawagonganisha RC Mongella, CCM
Habari za SiasaTangulizi

Matumizi mabaya ya fedha yawagonganisha RC Mongella, CCM

Spread the love

MGOGORO umeibuka Mwanza kati ya serikali ya mkoa na viongozi wa Chama cha Mapinduzi mkoa (CCM) kutokana na kile kinachotajwa kuwa ni kushindwa kusomwa kwa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2015. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mwanza … (endelea).

Mgogoro huo unadaiwa kuibuka baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella kushindwa kusoma taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kipindi cha mwaka 2017/18.

Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa chama hicho, zinasema CCM mkoa wa Mwanza imekuwa ikiomba kusomewa taarifa za utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM kutoka kwa mkuu huyo wa mkoa lakini hakuna majibu yeyote yanayotolewa.

Chanzo cha habari kutoka ndani ya uongozi wa chama hicho kinadai kuwa, sababu kubwa inayochangia Mongella kushindwa kusoma taarifa za utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kipindi cha 2017/18 ni kutokana na baadhi ya miradi kuwa mibovu.

Sababu nyingine zinazotajwa kuchangia kwa taarifa hiyo kushindwa kusomwa katika kikao maalumu cha kamati ya siasa mkoa ni kuchotwa kwa fedha za miradi ya maendeleo kwenye baadhi ya halmashauri za mkoa huo.

Chanzo hicho kilidai fedha zilizochukuliwa katika halmashauri hizo kwa amri ya mkuu huyo wa mkoa zilienda kumsaidia mmoja wa wagombea wa kiti cha uenyekiti wa CCM mkoa wa Mwanza, ambaye Mongella alikuwa akimpigia chapuo.

“Sisi kama viongozi wa chama tunafahamu kabisa fedha zilichukuliwa katika halmashauri za Buchosa, Misungwi, Nyamagana (Jiji) Sengerema na Ukerewe na ukiangalia kwenye hizo halmashauri kuna miradi mingi imekwama.

“Pamoja na kukwama kwa miradi hiyo, katika ripoti ya mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG) halmashauri hizo zimetajwa kwa matumizi mabaya ya fedha za umma na miradi yake kukwama kutokana na fedha kutumika katika matumizi ambayo hayakukusudiwa,” kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kiliendelea kueleza kuwa mkuu wa mkoa huo, baada ya kuona  viongozi wa CCM mkoa wameanza kuomba kusomwa kwa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo alianza kujenga uhasama  kwa baadhi ya viongozi wa ccm.

Aidha chanzo hicho kilisema kuwa, miongoni mwa viongozi ambao wanatajwa kuingia mgogoro na mkuu wa mkoa, ni Mwenyekiti wa CCM, Anthony Diallo ambaye kwa sasa inaelezwa yeye na Mongella ni kama paka na panya.

“Mongella ameshindwa kusoma taarifa za utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa mkoa wake lakini ukiangalia mikoa mingine tayari taarifa zimetolewa  na muda wa kusoma taarifa za utekelezaji wa miradi kwa mwaka huu umeisha.

“CCM ilimuagiza (Mongella) kupitia kwa kaimu katibu wa CCM mkoa wa Mwanza (Clement Mkondya,) kuomba kusomewa utekelezaji wa miradi ya maendeleo tumesubiri mpaka sasa hakuna majibu yeyote yale.

“Kama viongozi wa chama tunajiuliza inakuwaje mkuu wa mkoa anaagiza fedha za maendeleo zichukuliwe kwenye halmashauri kwa  ajili ya masuala ya kisiasa hili ndilo jambo linalowaumiza viongozi wengi.

Hata hivyo, chanzo hicho kilifafanua zaidi kwamba kiasi cha fedha ambazo zilichukuliwa katika halmashauri hizo ni zaidi ya Sh. 300 milioni na kwamba mamlaka zinazohusika zinapaswa kuchunguza tuhuma hizo.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mwanza, Anthony Diallo alipotafutwa na mtandao huu kupitia simu yake ya mkononi ili kupata ufafanuzi kuhusu mgogoro huo, alisema yupo nje ya mkoa huo na kwamba akirudi atalitolea ufafanuzi.

Mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella, alipotafutwa kupitia simu yake ya mkononi leo saa 08: 55 na saa 09: 03 asubuhi simu yake iliita bila kupokelewa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Rais Samia: Matumizi ya nishati safi sio anasa, ladha ipo

Spread the loveRAIS Samia Suluhu Hassan amesema matumizi ya nishati safi kwa...

Habari za SiasaTangulizi

Samia: Kuanzia Agosti marufuku kutumia mkaa, kuni

Spread the loveRAIS Samia Suluhu Hassan amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya...

Habari za SiasaTangulizi

Mwendokasi Kigogo – Segerea kujengwa awamu ya 5

Spread the loveNaibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Festo Dugange...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Rais Samia ni Mzanzibari: Shida Iko Wapi?

Spread the loveTAIFA linakabiliwa na upungufu wa fikra sahihi. Upungufu huu unaonekana...

error: Content is protected !!