Saturday , 27 April 2024
Home Kitengo Habari Kimataifa 500 wauawa katika shambulio la hospitali Gaza
KimataifaTangulizi

500 wauawa katika shambulio la hospitali Gaza

Spread the love

ZAIDI ya watu 500 wameripotiwa kuuawa usiku wa leo Jumanne kwenye shambulizi ambalo limetokea hospitalini Ahli Arab katika Ukanda wa Gaza. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa …(endelea).

Wizara ya afya ya Hamas imedai shambulizi la angani la Israel ndilo limesababisha maafa hayo. 

Lakini jeshi la Israel limekana kuhusika na kusema roketi ya Wanamgambo wa Kiislamu huko Gaza ndiyo imepiga hospitali.

Rais Mahmoud Abbas wa Palestina ametangaza siku tatu za maombelezo baada ya mashambulizi hayo, kwa mujibu wa mamlaka za ukanda huo.

Kulingana na Israel, intelijensia ya jeshi lake imebaini kuwa roketi iliyofyatuliwa vibaya na wanamgambo wa Gaza ndiyo ilishambulia hospitali ya Ahli Arab.

Kupitia taarifa ya Msemaji wa jeshi la Israel amedai kuwa tathmini ya mifumo ya operesheni ya jeshi lao inaonyesha kuwa msururu wa makombora ulirushwa na magaidi huko Gaza.

Amesema makombora hayo yalipita karibu na hospitali ya Al Ahli wakati iliposhambuliwa.

“Intelijensia tulizonazo kutoka vyanzo mbalimbali, zinaonesha wanamgambo wenye misimamo mikali ya Kiislamu, ndio wanawajibika kutokana na roketi iliyofeli na kupiga hospitali.”

“Kinachoendelea sasa ni mauaji ya kimbari. Tunaitaka jumuiya ya kimataifa kuingilia haraka kuzuwia mauaji haya ya maangamizi. Ukimya haukubaliki,” ilisema taarifa iliyotolewa na Chama cha Ukombozi wa Palestina (PLO) kinachoongozwa na Abbas.

Abbas na PLO walipoteza udhibiti wa Ukanda wa Gaza kwa kundi la Hamas baada ya uchaguzi wa 2006 uliofuatiwa na mapambano makali ya kuwania madaraka.

Haya yanajiri wakati rais wa Marekani Joe Biden akitarajiwa kuizuru Israel Jumatano, siku moja baada ya ziara ya Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz mjini Tel Aviv.

MASHAMBULIZI YALAANIWA

Shirika la Afya Duniani, WHO limelaani shambulizi hilo la Jumanne katika hospitali na kutaka ulinzi wa haraka kwa raia na vituo vya afya katika eneo hilo la Palestina.

“WHO linalaani vikali shambulizi katika hospitali ya Al Ahli Arab. Tunatoa wito kwa ulinzi wa haraka wa raia na huduma za afya, na amri za kuwahamisha ibadilishwe” amesema Tedros Adhanom Ghebreyesus, mkuu wa WHO, kupitia ukurasa wake wa X zamani ukijulikana kama Twitter.

Kulingana na Tedros, ripoti za awali zimesema mamia ya watu wameuawa na wengi wamejeruhiwa.

Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel, amesema mashambulizi dhidi ya miundombinu ya raia, haiendi sambamba na sheria ya kimataifa.

Mfalme Abdullah wa Jordan amesema shambulio dhidi ya hospitali huko Gaza ni mauaji ya kimbari na uhalifu wa kivita ambao yeyote yule hawezi kunyamazia kimya.

Wizara ya mambo ya nje ya Jordan imesema kuna haja ya watu wa Palestina kupatiwa ulinzi wa kimataifa na wakati huo huo ilitoa wito kuwepo juhudi za pamoja kuzuwia vita vinavyoendelea kwenye Ukanda wa Gaza.

Qatar imeyaita mashambulizi hayo kuwa ni mauaji ya kikatili ya maangamizi na uhalifu usio mfano dhidi ya raia wasiokuwa na ulinzi wowote.”

Saudi Arabia pia imelaani mashambulizi hayo. Kwenye taarifa yake, wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo imesema mashambulizi hayo ni “uvunjaji wa wazi wa sheria za kimataifa.”

Picha za televisheni zinaonesha mamia ya watu wakivutwa kutoka vifusi vya jengo la hospitali hiyo.

Tahadhari ya Israel kwa wakazi wa kaskazini mwa Gaza

Jeshi la Israel liliwaambia wakazi wa kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, takriban nusu ya idadi jumla ya watu milioni 2.4 katika ukanda huo, kuelekea kusini kwa usalama wao, kabla ya kuanza kwa mashambulizi ya ardhini.

Maelfu ya watu wamekuwa wakimiminika katika hospitali zilizofurika Gaza wakitafuta hifadhi kutokana na mashambulizi ya kijeshi ya Israel.

Israel imekuwa ikifanya mashambulizi katika Ukanda wa Gaza wakiwalenga wanamgambo wa Hamas, tangu kundi hilo lilipofanya mashambulizi makubwa ya kushtukiza dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba 2023.

Israel, Marekani, Umoja wa Ulaya na nchi nyingine kadhaa zimeliorodhesha kundi la Hamas kuwa la kigaidi.

Zaidi ya watu 1,400 wameuawa nchini Israel kufuatia mashambulizi hayo ya wanamgambo wa Hamas.

Katika Ukanda wa Gaza, zaidi ya watu 3,000 wameuawa kufuatia mashambulizi ya angani ya Israel.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoTangulizi

Jacob, Malisa waachiwa kwa masharti

Spread the love  JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam,...

Habari za SiasaKimataifaTangulizi

Tanzania, Somalia kuibua maeneo mapya ya ushirikiano

Spread the love  RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania na Somalia...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za SiasaTangulizi

Samia awataka watanzania kudumisha muungano

Spread the loveRais wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kuendeleza Muungano kwa...

error: Content is protected !!