WAGOMBEA Urais wa Tanzania na Zanzibar wa Chama cha Wananchi (CUF), katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020, kujulikana Jumatatu ya tarehe 27 Julai 2020. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Ratiba hiyo imetolewa leo Alhamisi tarehe 16 Julai 2020, na Juma Kilaghai, Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi CUF, wakati anazungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam.
Kilaghai amesema, wagombea hao watapatikana baada ya wajumbe wa mkutano mkuu, kuchagua jina moja kati ya majina ya wanachama waliojitokeza kutia nia kugombea nafasi hizo.
“CUF itafanya mkutano mkuu wa taifa maalum kwa ajili ya uchaguzi wa wagombea, tarehe 27 Julai 2020,” amesema Kilaghai.
Hadi sasa, Chief Lutalosa Yemba, mwanachama pekee wa CUF aliyejitosa kugombea urais wa Tanzania huku urais wa Zanzibar wakijitokeza watia watano.
Hata hivyo, bado dirisha la uchukuaji na urejeshaji fomu za kugombea urais wa Tanzania na Zanzibar ndani ya CUF litahitimishwa tarehe 18 Julai 2020.
Waliojitosa ni, Faki Suleiman Khatibu, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu CUF Zanzibar. Abbas Juma Mhunzi, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa CUF Zanzibar, Mhandisi Mohamed Habib Mnyaa, Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki.
Mussa Haji Kombo na Rajab Mbarouk, ni wanachama wa CUF waliojitokeza kutia nia kugombea Urais wa Zanzibar katika uchaguzi huo.
Kwa upande wa mchakato wa kuwapata wagombea ubunge, uwakilishi na udiwani katika uchaguzi huo, unatarajiwa kukamilika tarehe 24 hadi 25 Julai 2020, baada ya zoezi la uchukuaji na urejeshaji fomu kufungwa tarehe 18 Julai 2020.
“Mchakato wa ubunge, uwakilishi, udiwani na viti maalum unaendelea. Kura za maoni zimeanza siku tano zilizopita, tumepata asilimia 70 ya wagombea wote kwa upande wa bara. Tarehe 18 Julai zoezi litakamilika, wagombea wanapitishwa na Baraza Kuu la Uongozi,” amesema Kilaghai.
Leave a comment