December 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Membe akumbusha ‘machungu’ ya Lowassa, Sumaye

Spread the love

BERNARD Membe, mwanachama mpya wa Chama cha ACT-Wazalendo, amesema hatofuata nyayo za makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), waliohamia upinzani kisha kurejea katika chama hicho tawala. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Membe ametoa ahadi hiyo leo Alhamisi tarehe 16 Julai 2020, baada ya kupokelewa rasmi na chama hicho, katika ukumbi wa Mliman City jijini Dar es Salaam.

Mwanasiasa huyo amejiunga na chama hicho tarehe 8 Julai 2020 baada ya kufukuzwa na CCM tarehe 28 Februari 2020 akituhumiwa kukiuka miongozo ya chama hicho tangu mwaka 2014.

Waziri huyo wa zamani wa mambo ya nje katika utawala wa awamu ya nne chini ya Rais mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete, amesema yeye hatakuwa kama wale waliojiunga na upinzani kisha kurudi tena CCM.

Ingawa Membe hakuwataja kwa majina waliohamia upinzani kutoka CCM kasha baadaye kurejea CCM, lakini itakumbukwa mwaka 2015, mawaziri wakuu wastaafu Fredreck Sumaye na Edward Lowassa walitoka CCM na kujiunga na Chadema.

Lowassa alijiunga kasha kupitishwa kuwa mgombea urais wa Chadema na kuungwa mkono na vyama washirika wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya NCCR-Mageuzi, CUF, NLD na Chadema chenyewe.

Soma zaidi hapa

Membe akoleza moto urais Tanzania, atoa ombi Chadema

Hata hivyo, Lowassa baada ya kushindwa kuingia Ikulu, alitangaza kurejea CCM tarehe 1 Machi 2019 akipokewa na viongozi mbalimbali wa CCM wakiongowa na Mwenyekiti wa chama hicho, Rais John Pombe Magufuli katika ofisi ndogo za chama hicho, Lumumba, Dar es Salaam.

Pia, Sumaye alikwisha rejea CCM.

Katika mazungumzo yake, Membe amesema, “kuna watu wananiuliza wewe hautakuwa kama yule, wa kwenda na akarudi nyumbani? Hapa (ACT-Wazalendo) mimi ndio nyumbani kwangu, mimi ni mbele kwa mbele na ACT-Wazalendo ,” amesema Membe.

Soma zaidi hapa

Barua ya Membe yasomwa ukumbini

Membe amesema mazingira aliyoondoka yeye CCM hayafanani na wanasiasa waliowahi kuchukua hatua hiyo.

Benard Membe, Mwanachama mpya wa ACT-Wazalendo

Amesema yeye alifukuzwa uanachama wa CCM kwa fedheha, hivyo hawezi kurudi ili kulinda heshima yake.

“Na ni vizuri nikatuma ujumbe ufuatao, mazingira yaliyonifanya mimi niingie ACT ni tofauti kabisa na yaliyofanya mwenzangu aingie kule akarudi tena, wewe umefukuzwa na kesho unaenda tena? Jamani mimi nimefukuzwa tena kwa aibu, kwa fedheha na kutukanwa na vijana ambao ningeweza kuwazaa,” amesema Membe huku akishangiliwa

Akizungumza na wanachama wa ACT-Wazalendo katika mkutano huo, Membe amesema, “lazima tuingie Ikulu, mbinu tunazijua na sisi tutapindua.”

error: Content is protected !!