RAIS wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Ali Shein amesema utegemezi wa fedha katika bajeti ya serikali yake umepungua kutoka asilimia 30 alipoingia madarakani hadi kufikia asilimia 5.1 kwa mwaka wa fedha wa 2018/19. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).
Dk. Shein amesema hayo leo tarehe 12 Januari 2019, wakati akihutubia katika sherehe za maadhimisho ya miaka 55 ya mapinduzi ya Zanzibar iliyofanyika kwenye uwanja wa Gombani kisiwani Pemba.
“Utegemezi katika bajeti wakati naingia madarakani ulikuwa ni asilimia 30.2 Lakini kwa sasa umepungua hadi kufikia asilimia 5.1 kwa mwaka 2018/19 ikilinganishwa na asilimia 7.3 mwaka 2017/18,” amesema Dk. Shein.
Katika hatua nyingine, Dk. Shein amesema ukusanyaji mapato unaofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) umeongezeka kwa zaidi ya Sh. 100 bilioni, kutoka bilioni 512 mapato yaliyokusanywa mwaka wa fedha wa 2016/17 hadi kufikia Sh. 688.7 bilioni mwaka 2017/18.
Kuhusu kipato cha kila Mzanzibar kwa mwaka, Dk. Shein amesema kipato hicho kimepanda kutoka Sh. 1.8 milioni ambayo ni sawa na dola za Marekani 868 katika mwaka wa fedha wa 2016 hadi kufikia Sh. 2.2 milioni (dola 914) kwa mwaka 2017.
“Mafanikio hayo yametokeana na juhudi za serikali mbalimbali ikiwemo kuimarisha miundombinu ya kibiashara,” amesema Rais Shein.
Leave a comment