Saturday , 27 April 2024
Home Gazeti Tangulizi Rais Kikwete afuata nyayo za Mkapa
Tangulizi

Rais Kikwete afuata nyayo za Mkapa

Spread the love

RAIS mstaafu wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, ameanza kujiandikia kitabu kitakachoeleza historia ya maisha yake. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Kikwete amesema, katika kitabu hicho ataeleza vitu vingi alivyokutana navyo katika maisha yake ya kawaida na siasa.

Amesema, “kwenye kitabu hicho, nitaandika vitu vingi nilivyokutana navyo katika maisha yangu ya kawaida na siasa. Kitakuwa na mambo mengi  ambayo watu hawayafahamu watajifunza mengi.”

Kupatikana kwa taarifa kuwa Rais mstaafu Kikwete amepanga kuandika kitabu kinachoeleza maisha yake, kumekuja mwaka mmoja na miezi mitatu, tangu mtangulizi wake, Benjamin Mkapa, kuandika kitabu kinachoelezea historia yake.

Mkapa alifariki dunia, miezi nane baada ya kuzindia kitabu chake. Alikipachika jina la “Maisha Yangu, Kusudi Langu.”

Kitabu cha rais huyo mstaafu wa awamu ya tatu, kimeeleza historia ya maisha yake binafsi na yale ya kisiasa.

Mkapa alifariki dunia, tarehe 23 Julai 2020, kwa ugonjwa wa moyo, akiwa jijini Dar es Salaam. Alizikwa tarehe 29 Julai, kijijini kwake, Lupaso, wilayani Masasi mkoani Mtwara.

Rais John Magufuli akizindua kitabu cha Rais Mstaafu, Hayati Benjamin Mkapa, wengine ni wastaafu, Jakaya Kikwete na Ali Hassan Mwinyi

Akizungumzia kitabu hicho, Kikwete amesema, “nitaeleza maisha yangu,  sehemu nilizopitia na vitu nilivyojifunza. Nimejitahidi kuandika nilivyopitia, kuvisiikia na kuviona.”

Anaongeza, “nitakapomaliza kukiandika, kuna mambo mengi  ambayo watu hawayajui watayajua, kwa sababu katika maisha yangu,  sehemu nilizopitia kuna vitu vingi nilivyojifunza.”

Kiongozi huyo wa Tanzania katika Serikali ya awamu ya nne (2005-2015) amesema, katika kitabu hicho ataelezea historia ya muungano wa vyama vya Tanganyia African National Union (TANU) na Afro Shiraz Party (ASP) na kuanzishwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Amesema, “toka mwaka 1977 baada ya kuunganisha TANU na ASP nilipelekwa Zanzibar, sababu ni sehemu ya makao makuu ya CCM. Nimeshiriki karibu katika vikao vyote vya Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu (NEC), maamuzi mengi yalifanyika.”

Dk. Kikwete amesema, “kwa hiyo, kuna vitu vingi ambavyo nimeviona, nimevisikia na kushuhudia vikifanyika. Wakati mengine huwezi kuyasema, lakini kwa mengi nadhani hayana usiri huo. Nimejaribu kuchangia kwenye kitabu changu ninacho kiandika.”

Rais huyo mstaafu amesema, kupitia kitabu hicho, Watanzania watafahamu baadhi ya maamuzi yaliyofanyika katika nchi, ambayo yeye anayafahamu na aliyashuhudia.

“Hii itasaidia watu wengi kujua ilikuaje mpaka uamuzi huu ukafikiwa, au uamuzi huu ulifikiwa vipi, jambo hili chanzo chake ni nini mpaka tukafika hapa.  Kuna baadhi ya mambo nimesema mule, nadhani yatasaidia jamii kupata ufahamu wa baadhi yake,” ameeleza.

Akielezea kwa ufupi kuhusu historia ya muungano wa TANU na ASP, Kikwete amesema, alishiriki katika mchakato wa uunganishaji wa vyama hivyo, uliozalisha mfumo mmoja wa CCM.

“Katika mchakato wa kuunganisha TANU na ASP, mimi nilikuwa nashughulikia kuunganisha ile mifumo, kuihamisha ile mifumo ya TANU na ASP kuwa mfumo mmoja wa CCM. Ndio kazi nilikuwa naifanya pale,” amesimulia.

Amesema, yeye alikuwa mtu wa pili kutoka Tanzania Bara, kupelekwa Zanzibar ambapo alifanya kazi ya kuhamisha mifumo ya vyama hivyo kuanzia mwaka 1977 hadi 1980.

Ameongeza, “nilifanya kazi Zanzibar, walipounganisha TANU na ASP, wa kwanza kutoka Bara kupelekwa pale alikuwa Kanali Ayub Simba, akaenda kuwa Naibu Katibu Mtendaji Mkuu wa CCM.  Mimi ndio mtu wa pili kupelekwa pale.”

Sambamba na kusimamia uunganishwaji wa mifumo ya vyama hivyo, Rais Kikwete amesema, alikuwa msimamizi wa utawala katika ofisi kuu ya CCM Zanzibar, iliyoko Kisiwandui visiwani humo.

Jakaya Kikwete, Rais mstaafu wa Tanzania

Amesema, “nilifanya kazi ya kusimamia utawala pale makao makuu ya ofisi kuu ya CCM Kisiwandui, nimekaa pale mwaka 1977 mpaka 1980 ndio nikahamishiwa Dar es Salaam katika ofisi ndogo.”

Kuhusu historia yake ya siasa, Rais Kikwete amesema, alianza kujihusisha na siasa alipokuwa shule ya sekondari Kibaha, ambapo alijiunga na chama cha TANU.

Baada ya kushawishiwa na Christopher Lihundi, aliyekuwa Katibu Msaidizi wa chama hicho katika makao makuu ya umoja wa vijana wa chama hicho.

“Nilipoingia sekondari nikaanza ku-develop interest ya siasa pale Kibaha, ndio nilipojiunga na TANU, alikuja  Lihundi wakati huo alikuwa katibu msaidizi makao makuu ya umoja wa vijana TANU .

Alikuja shule ya sekondari Kibaha kutuhubiria na kutuhamasisha kujiunga na mimi nikajiunga na nilianza kuwa na maneno.

Amesema, baadae alikuwa mwenyekiti wa vijana wa TANU katika shule ya Sekondari Tanga. Kisha mwaka 1972, alipojiunga elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alichaguliwa kuwa kiongozi wa serikali ya wanafunzi chuoni hapo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari za SiasaTangulizi

Mpwa wa Magufuli mbaroni kwa kusambaza picha za utupu

Spread the loveJESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata...

Habari za SiasaTangulizi

Shibuda amlima waraka mzito Bulembo

Spread the loveMKONGWE wa siasa nchini, John Shibuda amemshukia kada maarufu wa...

error: Content is protected !!