Saturday , 27 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kubenea, Zitto, waisambaratisha Serikali kwenye Muswada wa Vyama vya Siasa
Habari za SiasaTangulizi

Kubenea, Zitto, waisambaratisha Serikali kwenye Muswada wa Vyama vya Siasa

Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi
Spread the love

MBUNGE  wa Ubungo (Chadema) Saed Kubenea amewavaa vigogo watatu wanasheria kuwa wamepeleka bungeni Muswada wa Marekebisho wa Vyama vya Siasa wa mwaka 2018, unavunja Katiba. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Kubenea amewavaa Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi na Mwasheria Mkuu wa Serikali Profesa Adelardus Kilangi na Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini Jaji Francis Mtungi wakati akichangia Muswada huo leo Januari 29 mwaka 2019.

“Sisi tusio wanasheria tunaona vifungu vinavyopingana na sheria. Tuliwaambia kuwa Rais atapoteza vyeo vyake kwenye muswada huu lakini wanachama wote wanaweza kupoteza uanachama lakini sio Rais,” amesema.

Kubenea amesema, muswada huo haukupita katika Baraza la Vyama vya Siasa; na kwamba baadhi ya wadau wakiongozwa na John Shibuda, mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, alitoa shukrani kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai kwa hatua yake ya kuwaita Dodoma ili kuweza kutoa maoni yao.

Shibuda ndiye mwenyekiti wa Baraza la vyama vya siasa kwa sasa.

Kwa mujibu wa Kubenea, mwenyekiti huyo wa baraza la vyama, aliwaeleza wajumbe wa Kamati kwenye mkutano uliowakutanisha wadau wengine, kuwa Jaji Francis Mutungi, alijichukulia mamlaka yote ya muswaada mikononi mwake.

“…mheshimiwa Spika, ndani ya kamati yako ya Bunge ya Katiba na sheria, baadhi ya wadau wakiongozwa na mheshimiwa Shibuda, walikushukuru sana kwa hatua yako ya kuwapa nafasi ya kushiriki katika muswaada huu. Ndani ya kamati, Shibuda alimtuhumu msajili wa vyama kutokana na hatua yake ya kulibeba jambo hili kama suala lake binafsi,” ameeleza Kubenea.

Katika hatua nyingine, Kubenea  amesema, ndani ya muswaada uliowasilishwa bungeni, kumewekwa mamlaka ya msajili wa vyama kuwa mlalamikaji, mwendesha mashitaka, jaji na bwana jela.

Amesema, “ndani ya muswaada, msajili wa vyama ndiye polisi, ndiye mlalamikaji, ndiye jaji na ndiye bwana jela. Haya hayakufanyika kwa bahati mbaya. Yamefanywa kwa makusudi kwa kuwa wahusika walikuwa na nia mbaya dhidi ya vyama vya upinzani na viongozi wao.”

Muswaada wa vyama vya siasa – The Political Parties (Amendment) Bill, 2018 – uliwasilishwa bungeni katika mkutano uliyopita wa Bunge na leo Jumanne, tarehe 29 Januari, ulianza kujadiliwa na baadaye kupitishwa kutokana na wingi wa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Naye Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe (ACT -Mzalendo), akichangia muswaada huo bungeni, alisema kuwa pamoja na mbwembwe nyingi zinazofanywa na wabunge wa CCM kutaka kuipitisha sheria hiyo, bado waathirika wakubwa watakuwa wao.

Alisema, miongoni mwa athari za wazi ambazo chama hicho kitapata, ni kufutwa kwenye daftari la msajili wa vyama vya siasa kwa kuwa CCM haikupitia mchakato wa usajili uliyopitia vyama vingine.

“Kwa hili mnalolifanya, siku ninyi mkipoteza udhibiti wa Bunge, hata kwa mbunge mmoja, yeyote atakayekuja, jambo la kwanza atakalolifanya, ni kuifuta CCM,” alieleza Zitto.

Katika mchango wake, Zitto alianza kwa kulikumbusha Bunge la Jamhuri kuwa mwaka 1933, aliyekuwa kiongozi wa Ujerumani, Adolf Hittler, alipeleka ndani ya Bunge la Ujerumani, Muswada wa Sheria ambao unaitwa Enabling Act.

Alisema, wabunge wa chama chake, isipokuwa chama kimoja cha SPT waliunga mkono muswaada huo, na kwamba ilichukua miezi sita tu baada ya kutungwa kwa sheria hiyo na kuanza kutumika, Ujerumani haikuwa na chama cha siasa.

Akiongea kwa uchungu, huku akimtolea macho Spika Ndugai, Zitto alisema, “Hittler alitumia sheria ile ile ambayo ilitungwa na Bunge la Ujerumani kuhakikisha sio tu vyama vimefutwa, bali wanasiasa ama wamekimbilia uhamishoni ama wameuawa kutokana na mazingira mabovu yaliyokuwa ndani ya sheria hiyo.”

Alisema, “na hii ndio hali mabyo Bunge lako tukufu inalo kwa sasa hivi, kwamba muswada hapa kwa nature ya majadiliano unaonekana ni muswada kati ya chama kinachotawala na vyama vya upinzani.

“Lakini utekelezaji wake na madhara yake yanakwenda zaidi ya ushindani wa chama kinachotawaka na vyama vya upinzani, kwa sababu sisi sote ni wanasiasa na tunajua mamlaka ambayo tunataka kumkabidhi msajili wa vyama vya siasa kwa mujibu wa sheria hii ni mamlaka yatakayotengeneza hali ngumu sana ya kisiasa katika nchi hii.”

Alimkumbusha Spika kuwa yeye ni mwalimu wa sheria, na kwamba taifa hili kabla ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi, na wakati wa utawala wa Mwalimu Julius Nyerere, kwa sababu watu hawakuwa huru kuzungumza kisiasa, kulikuwa na majaribio ya mapinduzi manane.

Alisema, “baada ya mfumo wa vyama vingi kuanza, nchi yetu haina rekodi ya jaribio la mapinduzi hata moja. Kwa sababu watu wakiwa na hasira wataenda Mwembe Yanga, wataenda Songea, watazungumza.

“Mazingira yanayojengwa sasa hivi, iwapo watu watakosa Uhuru wa ku-vent out na milango ikafungwa wakaamua kupita madirishani, tusilaumiane. Mheshimiwa Spika kuna hoja hapa ni wakati gani msajili wa vyama vya siasa anaweza akafuta chama, katiba yetu na imeelezwa vizuri, bahati nzuri mimi nilishiriki kikao cha kamati ya katiba na sheria na bahati nzuri Mwenyekiti aliniruhusu na tunampongeza sana mheshimiwa Chenge (Andrew) kwa kadri ya uwezo wake aliweza kuturudisha kila kifungu na vifungu vya kikatiba.

“Huwezi ukawa na katiba inayohusu freedom of association halafu ukawa na mtu ambaye unampa mamlaka peke yake ya kuamua kwamba kwa wakati huu sasa freedom of association inafutwa. Na katika hali ya kuonyesha kwamba inawezekana vyama vikafanya makossa, vikatakiwa kufutwa tulipendekeza ndani ya kamati kwamba pawepo na tribunal (mahakama ya vyama).

“Kwamba msajili anapoona chama kimefanya makosa, asiwe yeye tu aamue kuwe na tribunal, watu vyama vipelekwe kule, viweze kuwa trial na tribunal ile iweze kuamua, Mheshimiwa Spika muswada huu pamoja na marekebisho hakuna tribunal. Na best examples zimetajwa na mwenyekiti wa kamati.

“Ghana ambayo imezungumziwa kwa kina sana katika muswada huu kuna tribunal, Kenya ina tribunal, ni nini ambacho sisi tunakiona ni hatari kuweka tribunal ili kuhakikisha kwamba wote tunaona haki inatendeka. Naomba Mheshimiwa Spika na wabunge wenzangu walitazame hili, tuone uwezekano wa kufanya mabadiliko badala ya mamlaka haya tumemkabidhi msajili peke yake kuyafanya peke yake yaundiwe tribunal ambayo iweze kuyafanya na hiyo tribunal inateuliwa watu wa serikalini humo humo tu isi not a problem.

“Tunachokitaka kuwe na uwezo wa kuweza kuzungumza na kuweza kutoa maoni yetu kwa jinsi ambavyo inavyostahili, mheshimiwa Spika demokrasia sio uadui, na nchi yetu imefaidika sana na demokrasia, nikupe takwimu kidogo kati ya mwaka 2007 na mwaka 2012, jumla ya watanzania milioni moja waliondolewa kwenye poverty.

“Wewe unajua hiki ndio kipindi ambacho demokrasia ilikuwa imeshamiri sana katika nchi yetu, hiki ndio kipindi kulikuwa na upana zaidi wa mawazo, ndio kipindi ambacho serikali inakuwa responsible kwa watu wake.

“Data za juzi, ndani ya miaka mitatu toka utawala huu uingie madarakani watanzania milioni mbili wame-fall into poverty kwa sabu kati ya demokrasia na maendeleo ya watu, tunachopaswa kusema miaka 25 tangu tumeingia kwenye mf umo wa vyama vingi, sio kubana zaidi demokrasia, ni kuipanua zaidi demokrasia. Tungepaswa leo tuletewe muswada unaopanua zaidi badala ya kudhibiti.”

Naye mbunge wa Viti Maalum Salome Makamba (Chadema) amewataatharisha wabunge kuachana na tabia ya wabunge husuani wa Chama tawala kuacha tabia ya kupitisha sheria zenye alengo ya kuwakomoa wapinzania na badala yake watunge na kupitisha sheria kwa masilahi ya taifa.

Alisema siyo kweli kuwa CCM ni chama ambacho kitatawala milele bali ikumbukwe kuwa ipo siku chama hicho nacho kitaweza kuwa cha upinzani na kwa kutunga sheria mbovu kunaweza kusababisha sheria hizo kuwabana.

Kuhusu madaraka ambayo amepewa msajili alisema kuwa haiwezekani kutoa taarifa zote za chama kwa msajili kwani zipo taarifa nyingine za siri kwani ni mikakati ya chama husika kwa lengo la kuweka mipango ya kushika dola.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

error: Content is protected !!