Friday , 29 September 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Muswada Vyama vya Siasa wapita, wazua sintofahamu
Habari za SiasaTangulizi

Muswada Vyama vya Siasa wapita, wazua sintofahamu

Rais John Magufuli
Spread the love

BUNGE la Jamhuri, jana tarehe 29 Januari 2019, limepitisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa (2018), katikati ya msuguano mkali kati ya wabunge wa vyama vya upinzani na wale wa chama tawala. Anaripoti Danson Kaijage, kutoka bungeni mjini Dodoma…(endelea).

Kwa mujibu wa utaratibu, baada ya kupitishwa muswada huo ulioibua taharuki na mvutano mkubwa ndani na nje ya Bunge, sasa ni jukumu la Rais John Magufuli, kuusaini ili kuwa sheria.

Muswada wa mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa, uliwasilishwa bungeni jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu), Jenister Mhagama na baadaye mjadala kuanza, huku wabunge wote wa  upinzani wakiupinga na Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria, ikipinga baadhi ya vifungu.

Baada ya mvutano mkali, Bunge liliketi kama Kamati na ndipo mwenyekiti wake, Spika wa Bunge, Job Ndugai, aliongoza wabunge kupitia kifungu kwa kifungu. Baadaye alisema, “muswada umepita. Kilichobaki sasa, ni kuupeleka kwa mheshimiwa rais ili ausaini uwe sharia.”

Muswada huo umepitishwa huku taasisi mbalimbali zikiwa zimetoa maoni yake na kupendekezwa kufanyika marekebisho makubwa jambo ambalo kwa kiwango kikubwa mapendekezo hayo hayakufanyiwa kazi.

Mathalani, muswada uliweka vifungu vinavyolimbikiza mamlaka na madaraka kwa msajili wa vyama, ikiwamo kinga ya kutoshitakiwa mahakamani.

Baadhi ya wadau waliofika mbele ya Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria, walipinga susala hilo kwa maelezo kuwa haiwezekani kwa msajili kujiwekea kinga, wakati yeye amebeba roho za umma; na kwamba pendekezo hilo “linamfanya Msajili kuwa Mungu mtu.”

“Hapa kuna hila. Hakuna hiyo nia njema inayotajwa. Ndio maana msajili anahofia kupelekwa mahakamani. Kama angekuwa anaongozwa na dhamira njema, hili lisingekuwapo. Ndio maana anataka kinga. Nadhani kuna jambo baya ambalo analitaka kulifanya,” alieleza Dk. Vicenti Mashinji, katibu mkuu wa Chadema, wakati anatoa maoni yake.

Alisema, “ni bahati mbaya sana, kwamba sheria hii inasimamiwa na msajili ambaye ni jaji wa Mahakama Kuu. Hatua ya Jaji kuogopa mahakama, kunathibitisha kuwa kuna nia ovu.”

“Hata maoni ya Kamati na kile kilichokubaliwa na serikali ndani ya Kamati, hakikuletwa bungeni. Waziri Mhagama alileta vitu tofauti bungeni na vile alivyovileta ndani ya Kamati. Haya yalithibitika baada ya wajumbe kusoma taarifa ya mwenyekiti wa Kamati, jedwali la marekebisho na taarifa ya waziri,” ameeleza Ally Salehe, mbunge wa Malindi Unguja na mjumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria.

Akisoma maoni ya Kambi ya Upinzani, Msemaji Mkuu wa Kambi hiyo katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Ester Bulaya, aliainisha mapendekezo ya marekebisho kadhaa kuwa yanakinzana na Katiba ya Jamhuri na hivyo akaomba yaondolewe.

Bulaya alisema,“…Kabla hata ya kupitishwa kwa muswada huu, ambao kwa kiwango kikubwa unaharamisha na kufanya shughuli za kisiasa kuwa makosa ya jinai hapa nchini, tayari viongozi wa vyama vya siasa wamekuwa wakiandamwa na kesi za kisiasa wakiwemo takriban viongozi wote wa juu wa CHADEMA, Kiongozi wa ACT Wazalendo Mheshimiwa Zitto Kabwe na Mheshimiwa Seleamani Bungala  – Mbunge wa Kilwa Kusini.

“Ni vema Serikali hii ya CCM ikatambua kwamba siasa ni mfumo unaogusa maisha ya watu moja kwa moja. Kwa sababu hiyo, inapoleta muswada kandamizi kama huu, madhara yake hayatavikumba vyama vya siasa peke yake ambavyo serikali imepanga kuvidhibiti, bali yataathiri maisha ya wananchi kwa ujumla wake ikiwa ni pamoja na hata wale wasio na vyama.

Zitto aliingia Dodoma kwa ndege kutokea Dar es Salaam, ambako alikuwa anahudhuria shauri lake mahakamani.

Alisema, “Msajili ni mlezi wa vyama, katika hilo tulitarajia angalau alete muswada ambao utaweza kutatua mizozo baina ya viongozi ndani vyama, baina ya vyama na baina ya vyama na Serikali na au Tume ya Uchaguzi.”

Mbunge wa Mbinga Mjini (CCM), Sixtus Mapunda alisema, muswada huo ni mwarobaini wa matatizo mengi. Baadhi ya aliyota, hatua ya vyama kuunda vikosi vya ulinzi na kusema, makundi ya ulinzi ndani ya vyama baadaye hugeuka Mungiki na Al-Qaeda.

Hata hivyo, Mapunda hakulieleza Bunge kuwa makundi ya Green Gard yanayotuhumiwa kuvamia watu, kupiga na kujeruhi, katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, yalikuwa na mkono wake na kwamba kazi yote chafu iliyofanywa na makundi hayo, haiwezi kuwa imefanyika bila yeye kushiriki; na au kuibariki.

Naye Halima James Mdee, akichangia muswada huo alisema kuwa upinzani haujawahi kuogopa ukaguzi wa mahesabu yake na kwamba hoja ya ukaguzi wa ruzuku ililetwa bungeni na Zitto Zuberi Kabwe, takribani miaka minane iliyopita.

Alisema, “hatuogopi kukaguliwa. Hatujaogopa juzi, jana, leo na kesho. Sisi kupitia kwa mheshimiwa Zitto Kabwe, ndio tulileta hoja ya kutaka Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuvikagua vyama. Msipotoshe.”

Aliongeza, “lakini watu kupata hati chafu au hati ya mashaka, haiku kwa vyama tu. Safari hii, mtaona madudu. Tutaona jinsi madudu yalivyokuwa makubwa. Mtakimbia ninyi watu.”

Kwa upande wake, Saed Kubenea, mbunge wa Ubungo (Chadema) alishangazwa na vigogo watatu wanasheria kwa kuridhia kupelekwa bungeni Muswada wa Marekebisho wa Vyama vya Siasa wa mwaka 2018 kutokana na vipengele vyake kuvunja Katiba.

Kubenea alisema, “sisi tusio wanasheria tunaona vifungu vinavyopingana na sheria. Tuliwaambia kuwa Rais atapoteza vyeo vyake kwenye muswada huu lakini wanachama wote wanaweza kupoteza uanachama lakini sio Rais.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Serikali yawaangukia viongozi wa dini

Spread the loveSERIKALI imewaomba viongozi wa dini, waendelee kuelimisha wananchi kudumisha amani...

Habari MchanganyikoTangulizi

Afya ya akili yatajwa chanzo kuvunjika ndoa

Spread the loveCHANGAMOTO ya afya ya akili, imetajwa kuwa chanzo cha migogoro...

Habari za Siasa

Azzim Dewji aitaka Serikali iwanyooshe mafisadi

Spread the loveMFANYABIASHARA maarufu nchini, Azzim Dewji, ameitaka Serikali iwachukulie hatua wezi...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Kapinga: Usambazaji umeme vijijini mwisho Desemba 2023

Spread the love  NAIBU Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, amesema ifikapo mwezi...

error: Content is protected !!