Wednesday , 8 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Majaliwa awataka Watazania kubadilika, wapende vyao
Habari za Siasa

Majaliwa awataka Watazania kubadilika, wapende vyao

Spread the love

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wabadilike na wajifunze kujivunia kilicho chao. Anaripoti Mwandishi Wetu, Pwani … (endelea).

“Lazima tubadilike Watanzania, tuwe wazalendo, tukisemee kitu chetu, tujivunie kitu chetu na tujivunie ujuzi tulionao,” amesema.

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya waziri mkuu jana Jumanne tarehe 18 Agosti 2020 imesema, Majaliwa alitoa wito huo wakati akizungumza na viongozi mbalimbali wa mkoa na wafanyakazi wa kiwanda cha sukari cha Bagamoyo (BSL), katika kata ya Makurunge, wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani.

“Ninasema tubadilike sababu nimeenda kwenye maabara yao na kukuta wataalamu wetu wako vizuri, wanafanya utafiti wa udongo, maji na mbegu. Wameelezea vizuri utafiti wao na matokeo tumeyaona ni mazuri.”

“Rais wetu alisema Watanzania tunaweza, na leo nimethibitisha kwamba Watanzania tunao uwezo wa kazi lakini tatizo letu hatuwezi kujisemea wenyewe. Lazima tujisifu, tujisemee kuhusu umahiri tulionao. Ni kwa nini tujidharau?” alihoji.

“Nataka tubadilike sababu Watanzania tunaweza. Baadhi yao wanatoka hapa hapa Bagamoyo. Nimemuuliza ulisoma wapi, akajibu Chuo cha Kilimo Kaole, na hiki kiko Bagamoyo. Wengine wanatoka SUA (Chuo cha Kilimo cha Sokoine). Lazima turingie nchi yetu, lazima tuitangaze nchi yetu na ni lazima tuisemee nchi yetu,” amesisitiza.

Majaliwa alisema uamuzi wa Rais John Pombe Magufuli kutoa eneo hilo lenye hekta 10,000 ili lilimwe miwa na kujenga kiwanda cha sukari, ulilenga kuongeza uzalishaji wa sukari nchini.

“Tunahitaji kupata mashamba mengi ya miwa ili tuongeze uzalishaji wa sukari nchini,” alisema na kuongeza.

“Hivi sasa mahitaji ya suakri nchini yamefikia tani 450,000 kwa sukari ya mezani. Ile sukari ya viwandani ambayo inatumika kutengeneza soda, biskuti na pipi mahitaji yake ni tani 165,000 ambayo hapa nchini hatuizalishi, kwa hiyo inabidi tuiagize kutoka nje ya nchi.”

Alisema uzalishaji wa sukari ya mezani kwa sasa unafikia tani 380,000 kwa viwanda vyote vilivyopo na kwamba bado kuna bakaa ya tani 70,000.

Alisema mbali ya viwanda vilivyopo vya TPC, Kagera, Mtibwa, Kilombero, Manyara na Bagamoyo bado kuna maeneo ya kulima miwa huko Tarime na Kigoma. “Tunawaalika wawekezaji walime miwa na kuzalisha sukari zaidi.”

Akielezea kuhusu ujenzi wa kiwanda hicho, Majaliwa alisema ameridhishwa na kazi inayofanyika na kwamba kukamilika kwa mradi huo kutahakikisha sukari inapatikana kulekule na pia itatoa fursa ya kilimo cha miwa kwa wakazi wa maeneo jirani.

Aliwataka maafisa kilimo waende wakatoe elimu kwa wananchi kuhusu kilimo cha miwa.

“Wapeni uhakika wa soko ili wasisite kushiriki kwenye hiki kilimo. Wananchi watavutiwa wakijua kuna faida kwenye kilimo hicho lakini pia kiwanda kitapata tani za ziada na kuongeza uzalishaji wake,” alisisitiza.

Mapema, Mkurugenzi wa Makampuni ya Bakhresa, Abubakar Bakhresa alimshukuru Rais Magufuli kwa kuwapatia shamba hilo na kuahidi kuendana na dhamira ya Serikali ya kupunguza tatizo la upatikanaji wa sukari nchini.

Akielezea hatua zilizofikiwa kwenye mradi huo, Mkurugenzi wa Mahusiano wa Makampuni ya Bakhresa, Hussein Sufian alisema gharama ya mradi huo ni dola za Marekani milioni 100 na kwamba hadi sasa wameshapata asilimia 70 ya mtaji.

Alisema kampuni yao mpaka sasa imetoa ajira kwa watu 600 ambapo 500 kati yao wanatoka kwenye vijiji jirani vinavyozunguka eneo la mradi na kwamba mara baada ya awamu ya kwanza kukamilika, uzalishaji utakapoanza wataweza kuajiri watu 1,500.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Rais Samia ni Mzanzibari: Shida Iko Wapi?

Spread the loveTAIFA linakabiliwa na upungufu wa fikra sahihi. Upungufu huu unaonekana...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Mpina mwiba CCM, ahofia kuzibwa mdomo

Spread the loveWAKATI Chama cha Mapinduzi (CCM), kikijinasibu kuwa kinara wa demokrasia...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Mabeyo ametuepusha

Spread the loveNIMEGUSWA na uadilifu, utiifu na uaminifu wa Mkuu mstaafu wa...

Habari za SiasaTangulizi

CCM yaitaka TAKUKURU kuichunguza Chadema tuhuma alizoibua Lissu

Spread the loveCHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana...

error: Content is protected !!