SERIKALI imekiri kwamba kwenye Ukanda wa Pwani ya Tanzania kunapatikana madini ya aina mbalimbali ambayo ni barite, chokaa, chumvi, clay, dhahabu, flourite, jasi, kaolin, mchanga, mercury, niobim, ruby, rutile, titanium, zircon na gesi asilia, anaandika Dany Tibason.
Hayo yalielezwa leo bungeni na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medad Kaleman alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Rufiji, Mohammed Mchengerwa (CCM) ambalo liliulizwa kwa niaba yake na Mbunge wa Mkuranga, Abdallah Ulega (CCM).
Ulega alihoji kuhusina na maeneo mengi ya Pwani huwa na madini mengi, Je, eneo la Rufiji lina madini mengi ili wananchi hao washauriwe ipasavyo kutouza maeneo hayo.
Akijibu, Dk. Kalemani alisema ni kweli kwamba kwenye ukanda wa Pwani wa Tanzania kunapatikana madini ya aina mbalimbali ambayo ni pamoja na barite, chokaa, chumvi, clay, dhahabu, flourite, jasi, kaolin, mchanga, mercury, niobim, ruby, rutile, titanium, zircon na gesi asilia.
Amesema wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Kampuni ya Beak Consultants GmbH ya nchini Ujerumani ilifanya utafiti wa awali kati ya mwaka 2013 na 2014.
‘’Kutokana na utafiti huo madini yaliyobainika katika eneo la Rufiji ni pamoja na chokaa na niobium ambayo hupatikana katika eneo la Luhombero.
Pia alidai kuna viashiria vya uwepo wa Madini ya barite, dhahabu, flourite, mercury na sulfur katika maeneo ya Wingayongo karibu na Kibiti.
‘’Utafiti wa kina unahitajika ili kubaini kiasi halisi cha mashapo ya madini yaliyopo katika maeneo hayo,’’ amesema.
Leave a comment