June 22, 2021

Uhuru hauna Mipaka

IGP Sirro: Walipanga nchi isitawalike

IGP, Simon Sirro

Spread the love

MKUU wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro ameeleza kuwa, kuna watu walipanga wakati wa Uchaguzi Mkuu, nchi isitawalike. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).  

Bila kutaja jina la mtu ama kikundi, IGP Sirro amesema kitengo cha Intelejensia cha jeshi hilo, kilifanya kazi kubwa ikiwa ni pamoja na kukamata watu waliokuwa kwenye mpango huo.

“Kupitia intelijensia yetu, tulifanikiwa kukamata watu mbalimbali ambao lengo lao halikuwa uchaguzi bali kuhakikisha nchi haitawaliki, walitaka baadhi ya majengo kule Zanzibar na bara kuyaharibu, visima vya mafuta viweze kuharibiwa. Lengo walikuwa wanataka kuwe na vurugu na fujo mitaani ili kusudi labda wanaweza kupata uongozi,” amesema IGP Sirro.

Kauli hiyo ameitoa leo tarehe 19 Novemba 2020, wakati akizungumza na wanahabari kuhusu tathimini ya mchakato wa uchaguzi huo ambao umelalamikiwa na vyama vya upinzani.

Amesema, jeshi hilo lilikamata mabomu 10 ya kienyeji visiwani Unguja, ambapo wahusika baada ya kukamatwa, walikiri kutaka kuyatumia kuvuruga uchaguzi hasa kulipua Jengo la Ofisi za ZEC.

“Unguja tulifanikiwa kukamata mabomu 10 yaliyotengezwa kienyeji na baadhi ya watuhumiwa katika mahojiano, walikiri yaliandaliwa kufanya uharibifu jengo la ZEC na kuhakikisha visima vya mafuta vinasambaratishwa,” amesema IGP Sirro na kuongeza:

“Mtandao huo ulikua mpaka Bara watu waliandaliwa, jumla ya vijana70 walikuwa wamendaliwa kufanya hujuma kuhakikisha nchi haitawaliki, kuhakikisha kunakuwa na uharibifu mkubwa watu wanaingia barabarani kusiwe na amani.”

Akielezea tathimini ya uchaguzi huo, IGP Sirro amesema katika mchakato wa uandikishaji wapiga kura, hakukuwa na uvunjifu wa amani bali kulitokea vurugu katika wakati wa kampeni.

Ametaja maeneo yalikotokea vurugu kuwa ni Ukerewe mkoani Mwanza, Songwe, Kusini Pemba na Kaskazini Pemba na mkoani Mara.

Maalim Seif Sharrif Hamad, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo

“Kabla ya uandikishaji hatukuwa na matukio makubwa, shida kubwa ilikuwa katika kampeni, Ukerewe watu waliuawa, Songwe mtu aliuwa lakini wahusika walikamatwa.

“Kuna matukio Pemba Kaskazini kule msikitini, kuna watu walikatwa mapanga wanachama ambao ni wanachama wa CCM. Watuhumiwa walikamatwa,” amesema IGP Sirro na kuongeza:

“Kaskazini Pemba mtu mmoja alikatwa utumbo pia wahusika walikamatwa. Tarime Vijijini watu walipiga risasi wakauwa wawili lakini pia walikamatwa palepale. Kulikuwa na vurugu, matusi.”

Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi Tanzania amesema, vyombo vya ulinzi na usalama vilishughulikia matukio hayo na kwamba, waliohusika nayo baadhi yao wamekamatwa.

“Kwa mujibu wa takwimu zetu, matukio tuliyashughulikia vizuri lakini waliovunja sheria walikamatwa na kufikishwa mahakamani,” amesema IGP Sirro.

Amesema, watu 254 wako katika mahabusu katika vituo vya polisi mbalimbali nchini kwa tuhuma za uhalifu kabla, wakati na baada ya uchaguzi huo.

Akizungumzia malalamiko ya ukiukwaji wa haki za binadamu wakati wa uchaguzi mkuu, IGP Sirro amesema Jeshi la Polisi nchini, litafanya uchunguzi kwa maofisa wake wanaolalamikiwa kukiuka haki za binadamu.

Miongoni mwa tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu zilizotolewa na upinzani hasa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na ACT-Wazalendo ni mauaji na uteswaji wa wafuasi wake, visa vinavyodaiwa kufanywa na maofisa wa polisi.

Amesema, Jeshi la Polisi likiongozwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI), litafanya uchunguzi kubaini askari polisi waliotumia nguvu katika mchakato huo.

IGP Sirro amesema, uchunguzi huo ukikamilika watakaothibitika kuhusika na makosa hayo, watachukuliwa hatua na kwamba, askari hao watachukuliwa hatua pamoja na watu watakaobainika kufanya uvunjifu wa sheria katika uchaguzi huo.

“Uchunguzi unaendelea, niwahakikishie walioshiriki watachukuliwa hatua lakini askari wetu wanafuatilia kama kuna askari walitumia nguvu kupita kiasi watachululiwa hatua, DCI ataongoza hilo,” amesema IGP Sirro.

error: Content is protected !!