Saturday , 27 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Dk. Masumbuko Lamwai, afariki dunia
Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Dk. Masumbuko Lamwai, afariki dunia

Spread the love

DK. Masumbuko Mahunga Selasini Lamwai, aliyepata kuwa mbunge wa Ubungo (NCCR -Mageuzi) na mbunge wa kuteuliwa na Rais, mwanasheria nguli nchini, amefariki dunia. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Dk. Lamwai amefariki dunia majira ya saa sita za usiku wa jana Jumatatu, jijini Dar es Salaam.

Taarifa za kifo chake, zimetibitishwa na mdogo wake, Joseph Selasini. Joseph na Masumbuko, ni ndugu wa damu kwa baba na mama.

Selasini amesema, kaka yake huyo alizidiwa jana usiku na kupelekwa hospitali ya Rabininsia Memorial iliyopo Tegeta, jijini Dar es Salaam.

“Alipofika pale, wale madaktari wakawaambia huyu bwana ameshafariki. Inaonekana amekutwa na mauti, ama akiwa nyumbani au njiani wakati anapelekwa hospitali,” ameeleza Selasini ambaye ni mbunge wa Rombo, mkoani Kilimanjaro.

Katika kipindi cha uhai wake, Dk. Lamwai alikuwa mmoja wa vigogo wa upinzani nchini, ingawa baadaye mwaka 2000 alijiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mwaka 1994, Dk. Lamwai alijitosa katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa udiwani katika kata ya Manzese, jimboni Ubungo. Akashinda na kuwa pekee wa upinzani wa kwanza mkoani Dar es Salaam.

Hakuishia hapo. Pamoja na kuwa diwani pekee wa upinzani, Dk. Lamwai aliamua kujitosa katika kinyang’anyiro cha kugombea umeya wa Jiji la Dar es Salaam, ambako aliambulia kura moja!

Akijibu swali la mmoja wa waandishi wa habari, kwamba kwa nini amegombea umeya huku akijua yupo peke yake na atashindwa?

Alijibu: “Nilitambua hilo, lakini sikutaka kupata dhambi kwa kumpigia kura mgombea wa CCM. Kumpigia kura mgombea wa CCM, kwangu ni dhambi kubwa.”

Baadaye Dk. Lamwai alisema, wale waliomnyima kura za kuwa Meya wao wa Jiji, wakipata wageni kutoka nje hna ambao hawafahamu Kiswahili, walikuwa wanamuita yeye kuwakilisha.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995, Dk. Lamwai alijitosa kuwania ubunge katika jimbo la Ubungo. Akashinda na kuwa mbunge wa kwanza wa upinzani jijini Dar es Salaam, kupitia NCCR- Mageuzi.

Dk. Lamwai alijitosa katika kinyang’anyiro cha ubunge, wakati chama chake, kimewazuia wagombea wake kushiriki uchaguzi wa marudio, kufuatia kufutwa kwa uchaguzi wa kwanza katika mkoa mzima wa Dar es Salaam.

Dk. Lamwai atakumbukwa kama mwanasiasa machachari, mwanasheria nguli na mkufunzi mwandamizi (senior lecturer) wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Tumaini.

Ndani ya NCCR-Mageuzi, alikuwa na wanasiasa wengine wakongwe kama vile Mabere Marando, Prince Bagenda, Anthony Komu, Dk. Sengondo Mvungi, Augustine Mrema, Dk. Ringo Tenga, Ndimara Tegambwage, Prof. Mwesiga Baregu, Dk. Haidar Maguto, James Mbatia, James Nyakyoma na wengineo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari Mchanganyiko

Wakili: Ukimpa zawadi mwenza marufuku kumpora hata mkiachana

Spread the love  WANANDOA na watu waliko kwenye mahusiano ya kimapenzi, wamekumbushwa...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

error: Content is protected !!