KIONGOZI wa Chama Cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema chama chake kinaendelea kumuenzi aliyekuwa Mwenyekiti wake Taifa, Maalim Seif Shariff Hamad, aliyefariki Dunia tarehe 17 Februari 2021. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Akitoa ujumbe wake wa kumbukumbu ya miaka miwili ya kifo Cha Maalim Seif, leo tarehe 17 February 2023, kupitia ukurasa wake wa Twitter, Zitto amesema ACT-Wazalendo itaendeleza harakati zake kuimarisha demokrasia na kupigania muungano wa haki nchini.
“Tunakuenzi kwa kuendeleza harakati za kuimarisha demokrasia nchini na kupigania muungano wa haki, heshima na usawa. Tunaendelea kusimamia maridhiano ya Wazanzibari na kuongoza juhudi za maridhiano ya Watanzania. Tunakukumbuka kwa vitendo Maalim!,” ameandika Zitto.
Maalim Seif pamoja na wafuasi wake, walijiunga na ACT-Wazalendo 2019, kupitia opereshenj yake ya shusha tanga, pandisha tanga, wakitokea Chama cha Wananchi (CUF), baada ya kukosa muafaka katika mgogoro wa kiuongozi uliokuwa unakikabili chama hicho, baada ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, kumtambua Prof. Ibrahim Lipumba, kuwa mwenyekiti halali.
Leave a comment