Sunday , 28 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Watanzania wawili ni miongoni mwa mateka wa Hamas
Habari MchanganyikoTangulizi

Watanzania wawili ni miongoni mwa mateka wa Hamas

Spread the love

 

RAIA wawili wa Tanzania na mmoja wa Afrika Kusini, ni miongoni mwa mateka 224, wanaoshikiliwa na wanamgambo wa Hamas, baada ya mashambulizi ya tarehe 7 Oktoba nchini Israeli. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa ya serikali mjini Tel Aviv, nchini Israeli, inasema, takribani wageni kutoka nchi 25, ikiwamo Marekani na mataifa mengine, bado wanazuiliwa na Hamas.

Hata hivyo, taarifa hiyo, haikutaja jina la raia hata mmoja kati ya hao watatu.

Lakini ubalozi wa Tanzania nchini Israeli, imeeleza mara kadhaa kuwa haifahamu waliko raia wake wawili, wanaoishi kusini mwa nchi hiyo, ambalo lilishuhudia mapambano baina ya wanamgambo wa Hamas pamoja na jeshi la taifa hilo.

Mmoja wa wanaotaja kutokuwa na mawasiliano na ubalozi, ni Joshua Loitu Mollel, ambaye baba yake mzazi Loitu, alinukuliwa akiiambia BBC, kwamba mara ya mwisho kuwasiliana na mwanawe, ilikuwa 5 Oktoba.

Alisema, hafahamu Joshua yuko katika hali gani na kwamba alikuwa anaendelea kusubiri taarifa kutoka kwenye mamlaka za serikali nchini.

Joshua (21), ni mwanafunzi wa kilimo kwenye mojawapo ya eneo makazi la Kibbutz Nahal Oz, ambalo lilishambuliwa na Hamas. Alikuwa ameondoka nchini mwezi mmoja uliyopita.

Mateka hao walichukuliwa wakati wanamgambo kutoka Hamas – ambao Israeli, Uingereza, Marekani na kundi la mataifa yenye nguvu yanaitaja kama shirika la kigaidi – walipovuka hadi Israel kutoka Gaza na kuingia Israeli, ambako liliteketeza takriban watu 1,400.

Tangu wakati huo, Israeli imelipiza kisasi kwa mashambulizi ya anga huko Gaza, ambayo wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas inasema yameua takriban watu 6,500.

Hatua ya Hamas ya 7 Oktoba, kuuvamia mji wa Kibbutz Nahal Oz, umbali wa mita 800 kutoka Gaza, iliishangaza ulimwengu.

Taarifa kwamba Israel imevamiwa na Hamas ilipotangazwa, nilijaribu kufuatilia kujua iwapo Israel ina ubalozi Tanzania lakini nikaambiwa wanafanya kazi kutoka Kenya.

Baba mzazi wa Joshua anasema, “baada ya hapo niliwasiliana na wizara ya mambo ya nje ya Tanzania na hata balozi wa Tanzania aliyeko Tel Aviv. Lakini bado sijapata taarifa kuhusu mtoto wangu yuko wapi na yuko katika hali gani.”

“Tunafanya kazi kwa ushirikiano mamlaka ya Israel ili kubaini walipo wanafunzi hao wawili waliotoweka,” anasema balozi wa Tanzania mjini Tel Aviv, Alex Kallua.

Takriban Watanzania 350 wanaishi Israeli, asilimia 70 kati yao wakiwa wanafunzi wengi wakisomea mambo yanayohusiana na kilimo, kulingana na maafisa wa Tanzania.

Balozi Kallua anasema, Watanzania tisa wamerejea salama nyumbani wiki moja iliyopita, na kwamba wafanyakazi wa ubalozi wake “wako makini na wanawasiliana na Watanzania wengine [ambao bado] wako Israeli na kuhakikisha wote wako salama.”

Familia ya Joshua inasema mafunzo yake katika shamba la ngo’ombe wa maziwa la Nahal Oz nchini Israel yaliandaliwa na chuo chake kilichopo katikati mwa Tanzania, Taasisi ya Mafunzo ya Wizara ya Kilimo – Katrin.

“Hatutaki kulaumu mamlaka kwa kuendesha polepole mpango wa kumtafuta mjukuu wangu, kwa sababu tunaelewa baadhi ya maeneo ya Israel yalishambuliwa na Hamas,” babu yake Joshua, Ephata Nanyaro, anasema kidiplomasia.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mavunde aibana kampuni kutimiza masharti ya mkataba

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameitaka Kampuni ya Xin Tai...

Habari Mchanganyiko

Dk. Jafo aipongeza Oryx kumuunga mkono Samia

Spread the loveWAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na...

Habari Mchanganyiko

Mvungi aendesha kikao kazi cha wataalam wa Regrow

Spread the love  MKURUGENZI wa Idara Sera na Mipango Wizara ya Maliasili...

Habari MchanganyikoTangulizi

Jacob, Malisa waachiwa kwa masharti

Spread the love  JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam,...

error: Content is protected !!