July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Watanzania kuiwakilisha Afrika mashindano ya TEHAMA ya Huawei Duniani

Spread the love

WANAFUNZI kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ni miongoni mwa washiriki wa fainali za Mashindano ya kimataifa ya TEHAMA kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara yanayoandaliwa na Huawei chini ya kauli mbiu ya “Connectivity, Glory, Future”. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Katika hatua ya awali (kanda ya kusini mwa Afrika) ya mashindano hayo wanafunzi kutoka Tanzania waliibuka washindi kwa kushika nafasi ya kwanza, pili na tatu na hivyo kukata tiketi kuuwakilisha ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara katika Mashindano ya Dunia.

Fainali za dunia za mashindano hayo zinatarajia kufanyika kwa njia ya mtandao siku ya Jumamosi tarehe 18 Juni 2022.

Katika hatua hiyo timu 102 kutoka mataifa Zaidi ya 40 zitachuana katika teknolojia za kisasa kabisa. Ambapo ukanda wa Jangwa la Sahara utawakilishwa na timu kutoka Tanzania, Nigeria, Ghana, Kenya, Mauritius, Uganda na Zimbabwe.

Tanzania inashiriki hatua ya fainali kwa ngazi ya dunia kwa mara ya pili, huku ikiwa na kumbukumbu nzuri ya fainali zilizopita kwa kuibuka mshindi wa pili katika fainali hizo.

Akizungumza kwa niaba ya timu zitakazoiwakilisha Tanzania Zuwena Salum kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amesema kuwa wamefanya maandalizi ya kutosha na wanaamini kuwa watafanya vizuri katika fainali hizo.

‘‘Tumepata muda mzuri wa kujifunza na kufanya majaribio mara kwa mara, tuna Imani na namna ambavyo tumejiandaa, mbele yetu tuna jukumu kubwa moja tu nalo ni kuithibitishia dunia kuwa Tanzania ina vipaji vya kipekee katika masuala ya teknolojia’’ amesema.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. James Mdoe, pamoja na kuwapongeza, ameeleza matumaini yake juu ya wawakilishi hao wa Tanzania katika mashindano hayo makubwa duniani na kuwatakia heri katika fainali hizo.

‘‘Inatia moyo sana kuona wanafunzi wetu wa vyuo vikuu vya hapa nyumbani wakishiriki kikamilifu katika Mashindano ya TEHAMA ya kimataifa, na timu nyingine kutoka duniani kote.

Najivunia wanafunzi wetu, naamini katika uwezo wao na niko tayari kusikia habari njema jumamosi hii. Nawatakia heri, Kazi iendelee!

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Msaidizi wa kampuni ya Huawei Tanzania, Tom Tao amesema anaamini Tanzania ina vijana bora na wenye vipaji vya hali ya juu hivyo, anatarajia kuwa timu kutoka Tanzania itaibuka kidedea katika fainali hizo.

Shindano la TEHAMA linaloandaliwa na Huawei, kwa mwaka huu limeshirikisha zaidi ya nchi 85 Ulimwenguni kote, na kushindanisha wanafunzi 150,000 kutoka vyuo zaidi ya 2000.

Tangu kuzinduliwa kwake miaka sita iliyopita, Shindano la TEHAMA la Huawei limeendelea kukua na kuwa shindano kubwa Zaidi la TEHAMA barani Afrika.

error: Content is protected !!