July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

WFP kununua tani 40,000 za mazao

Wakulima wa mahindi bora Kata ya Gwarama wilayani Kakonko mkoani Kigoma wakiwa wanaonesha mahindi walifikisha kwenye chama chao cha ushirika

Spread the love

 

SHIRIKA la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) linararajia kununua tani 43,000 za mahindi, maharage na mtama kwa wakulima kutoka mikoa mbalimbali. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kigoma … (endelea).

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Ofisi ya WFP Kibondo, Saidi Johari wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii mwishoni mwa wiki.

Johari alisema WFP inatarajia kununua maharage tani 3,000, mahindi tani 30,000 na mtama tani 10,000 ambayo yatasambazwa kwa wakimbizi na nchi nyingine.

Alisema WFP inanunua mazao ambayo yana ubora unaokubalika kimataifa ndio maana wanashirikiana na mashirika mengine yanahusiana na kilimo.

“Mwaka huu tumejipanga kununua tani 43,000 za mazao ya mahindi, mtama na maharage ambayo yatakidhi bigezo ambapo kwa Kigoma asilimia kubwa ya mazao wanayolima yamefikia viwango,” alisema.

Mkuu huyo wa ofisi alisema shirika hilo linatarajia kununua mazao hayo kwa bei ambayo inaridhisha wakulima kupitia vyama vyao vya ushirika.

Mkuu wa Ofisi ya Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Wilaya ya Kibondo, Saidi Johari akielezea walivyomuinua mkulima wilayani hapo

Aliwataka wakulima nchini kulima kilimo ambacho kinafuata taratibu ili kuwa na uhakika na soko la mazao yao kwa WFP na wadau wengine.

Johari alisema WFP Mkoa wa Kigoma inashiriki katika Programa ya Kigoma Pamoja (KJP) ambao unashirikisha mashirika 16 ya Umoja wa Mataifa (UN), huku wao wakijikita katika kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Wilaya ya Kibondo, Kanali Aggrey Magwaza alipongeza WFP na mashirika mengeo ya UN ambayo yanashiriki katika kuongeza thamani ya mazao ya chakula wilayani hapo.

Kanali Magwaza alisema ujio wa mashirika hayo umeongeza uzalishaji wa mazao ya maharage na mahindi wilayani hapo hali ambayo inaongeza mapato kwa Serikali na wakulima.

“Sisi tunawapongeza WFP na wenzao kuja Kibondo, kwani matokeo yake yameweza kuonekana kwa muda mchache, niwaombe muendelee kutoa mafunzo ya kilimo bora kwa maeneo mengine,” alisema.

Magwaza alisema mashirika hayo yamewezesha kuondoa watu wa katikati ambao walikuwa wananunua mazao kwa bei ndogo inayoumiza wakulima na kuikosesha Serikali mapato.

Mkulima Agnes Christopher wakianza kulia, Esther Makere na Winfrida Mkwabi wakisambaza maharage ambayo yamefikishwa na wakulima kwenye Chama cha Ushirika Muungano Kiziguzigu wilayani Kakonko mkoani Kigoma

Alisema wao kama wilaya wamejipanga kutumia wataalam wa kilimo na kushirikiana na wakulima waliopata mafunzo kuendelera kupata mafunzo ambayo yataongeza chachu ya uzalishaji.

“Tunataka vijiji vyote vifanye kilimo ambacho kina tija na hilo litafanikiwa kwa kuwekeza kwenye elimu ya mbinu bora za kilimo,” alisema.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Evance Mallasa alisema WFP kupitia mradi wa KJP imefanya mapinduzi ya kilimo wilayani hapo na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa wadau wote.

Kanali Mallasa alisema sekta ya kilimo ikipewa kipaumbele itaweza kuwakomboa wananchi wengi wa vijiji ambao wanajihusisha na kilimo.

error: Content is protected !!