May 20, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wanawake ACT wamvaa JPM

John Magufuli, Rais wa Tanzania

Spread the love

NGOME ya Wanawake ya Chama cha ACT –Wazalendo imemtaka Rais John Magufuli atengue kauli yake kuhusu marufuku ya wanafunzi wanaopata ujauzi kurejea masomoni baada ya kujifungua, anaandika Pendo Omary.

Siku tatu zilizopita Rais Magufuli alishtua wengi kwa kutangaza kuwa kamwe utawala wa serikali yake hautaruhusu mwanafunzi yoyote aliyepata ujauzito kurejea masomoni baada ya kujifungua, akisema serikali yake haipo tayari kusomesha wazazi.

Esther Kyamba, Katibu Ngome ya Wanawake ACT Wazalendo, kauli ya Rais Magufuli ukandamizaji na ubaguzi wa wazi kwa mtoto wa kike, kwani marufuku hiyo inalenga kumnyima mtoto wa kike haki ya msingi ya kupata elimu.

“Marufuku hii ni kinyume cha matakwa ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 11(2) inayosema: Kila mtu anayo haki ya kujielimisha, na kila raia atakuwa huru kutafuta elimu katika fani anayopenda hadi kufikia upeo wowote kulingana na stahili na uwezo wake,” amesema Kyamba.

Pia Kyamba amesema licha ya kuzuia haki ya kikatiba ya kujielimisha kwa mtoto wa kike lakini pia Rais ametumia mamlaka yake kumbagua mtoto wa kike katika haki zake za msingi kinyume na Ibara ya 13(4) ya katiba inayosema kuwa “Ni marufuku kwa mtu yeyote kubaguliwa na mtu au mamlaka yoyote inayotekeleza madaraka yake chini ya sheria yoyote au katika utekelezaji wa kazi au shughuli yoyote ya Mamlaka ya Nchi.”

Ameongeza kuwa, marufuku hiyo pia ni kinyume na Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009 (The Law of Child ACT, 2009) Ibara ya 5 (1) inayosisitiza kuwa “Mtoto ana haki ya kuishi huru bila kubaguliwa.”

“Rais atambue kuwa Tanzania imeridhia na kusaini maazimio mbalimbali ya kimataifa kuhusu haki za mtoto wa kike kama vile Azimio la Dunia la Haki za Binadamu la mwaka 1948 (Universal Declaration on Human Rights (1948) ibara ya 26(1).

“Pia tamko la Kimataifa la kupinga aina zote za ukandamizaji dhidi ya Wanawake (Convention of the Elimination of all forms of Discrimination Against Women – CEDAW) la mwaka 1979 ambayo yote yameweka msisitizo wa kulinda haki za mtoto wa kike,” amesema.

Aidha, amesema inashangaza kuona Rais aliyefanya kampeni mwaka 2015 Kwa kutumia ilani ya uchaguzi ya CCM iliyoahidi kuwa CCM ikifanikiwa kuunda Serikali itaruhusu wanafunzi wa kike wenye ujauzito kurudi shuleni baada ya kujifungua lakini kwa sasa anatenda kinyume na ilani hiyo.

“Hii inaonesha kuwa Rais aliwalaghai wananchi kwa nia ya kupata kura. Zipo changamoto za kiuchumi, kijamii na kimazingira zinazomkabili mtoto wa kike na zinazochangia kwa kiasi kikubwa kumuingiza katika matatizo ya kupata ujauzito akiwa shuleni,” amesisitiza Kyamba.

error: Content is protected !!