August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Takukuru wafunguka kushikiliwa kwa Malinzi, Mwesigwa

Jamal Malinzi, Rais wa TFF akiwa na Katibu wake, Selestine Mwesigwa

Spread the love

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imethibitisha kuwachunguza Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na Katibu wa TFF, Selestine Mwesigwa, lakini hawajakubali wala kukataa kama wamewashikilia, anaandika Mwandishi Wetu.

Taarifa za kushikiliwa kwa Malinzi na Mwesigwa zilianza kusambaa mitandaoni lakini hakukuwa na mtu aliyetoa uthibitisho juu ya hilo.

Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Takukuru, Musa Misalaba amesema ni kweli Takukuru wanafanya uchunguzi wa rushwa katika shirikisho hilo lakini hakukiri kuwa ni kweli kama wamewashikilia viongozi hao au la.

Misalaba amesema kuwa ni kweli kumekuwa na madai ya rushwa lakini suala la kusema kama wamewashikilia vigogo hao au wamefikia wapi, bado ni mapema wao kusema lakini watatoa taarifa mambo yote yatakamilika.

“Sisi hatujasema kama tumemshika mtu yeyote, ni kweli tunafanya uchunguzi lakini kwa sasa ni siri yetu, kila kitu kitakapokuwa tayari tutaweka, unajua suala la rushwa lina mazingira mengi, kuhusu wamefanya nini, hilo ni jukumu letu,” amesema Misalaba na kuongeza: “Sheria hazituruhusu kusema kwa sasa, muda ukifika tutasema.”

Kwa upande wa TFF, Makamu wa Rais wa shirikisho hiyo, Warles Karia amesema hana taarifa ya kushikiliwa kwa viongozi wenzake hao, kwani hajawasiliana nao hivi karibuni na huwa hana utaratibu wa kuwasiliana nao mara kwa mara.

“Mimi kwa sasa nipo Morogoro na sijui lolote juu ya taarifa hizo. Nami nimepata taarifa hizo kupitia mitandao ya kijamii. Kama tukio hilo likiwa limetokea kweli litajulikana tu, maana TFF kuna msemaji wake,” amesema Karia.

error: Content is protected !!