May 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wanaotiririsha majitaka Mabibo wapewa siku 7

Spread the love

 

MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) na Manispaa ya Ubungo, wametoa siku saba kwa wananchi wanaotiririsha majitaka katika mabwawa ya Mabibo kujisalimisha. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mamlaka hizo zimesema, wahusika wote, wajisalimishe Manispaa au Dawasa na wale watakaokaidi agizo hilo ndani ya muda huo uliotolewa, hatua kali za kisheria zitachukuliwa.

Hilo limesemwa jana Jumatatu tarehe 12 Julai 2021 na Afisa Afya kutoka Manispaa ya Ubungo, Ndugu Ezra Guya katika kikao kazi, kilichohusisha Dawasa, Manispaa na watendaji wa mtaa wa Mabibo.

Kikao hicho, kilichokuwa na lengo la kuboresha huduma za majitaka jijini Dar es Salaam.

Ndugu Guya amesema, ni wakati muafaka kwa mamlaka zinazosimamia usafi wa mazingira kuweka sheria na miongozo itakayolinda mazingira na kuepusha madhara yanayotokana na uchafuzi wa mazingira kama vile magonjwa ya mlipuko na harufu mbaya.

Amesema, wamepokea malalamiko ya wakazi wa Mabibo wanaozunguka Mabwawa ya kuchakata majitaka kutiririsha majitaka kwenye mitaro ya maji ya mvua na kuyapeleka katika mabwawa ya majitaka Mabibo yanayosimamiwa na DAWASA.

“Tabia hii kwa wananchi wa mabibo sio sahihi, lazima likemewe upesi na kwa haraka. Mitaro hii ya maji ya mvua isiruhusiwe kutumika kupitisha majitaka kwani madhara yake ni makubwa kwa jamii hasa magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu,” amesema Ndugu Ezra.

Kwa upande wa DAWASA, Mhandisi Rose Edward amesema, zaidi ya kaya 60 zinazozunguka Mabwawa ya Majitaka Mabibo, wanatiririsha Majitaka na kutupa taka ngumu katika miundombinu hiyo jambo ambalo ni kinyume na sheria za kanuni za afya.

“Kwanza tumeanza utaratibu wa kuwaondoa wananchi waliovamia na kujenga ndani ya eneo la mabwawa haya,” amesema Mhandisi Rose na kuongeza:

“Vilevile kwa wale waliopo kwa mujibu wa sheria tutaweka utaratibu sahihi wa matumizi ya miundombinu hii ili isilete uharibifu kama vile kuwajengea mifumo rahisi ya ukusanyaji na uondoshaji majitaka katika makazi ya watu.”

DAWASA ina jumla ya mabwawa saba ya kuchakata Majitaka ambayo ni ya Mabibo, Mikocheni, Vingunguti, Kurasini, Airwings, Lugalo na Vingunguti.

error: Content is protected !!