SERIKALI ya Afrika Kusini imelazimika kuingiza Jeshi mtaani, ili kutuliza ghasia zilizoanzishwa na wafuasi wa rais mstaafu wa nchi hiyo, Jacob Zuma (79), wakipinga mwanasiasa huyo kufungwa miezi 15 gerezani. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).
Ghasia hizo ziliibuka jana tarehe 12 Julai 2021, katika Mkoa wa Gauteng na KwaZulu –Natal, mkoa anaotoka Zuma, ambapo wafuasi hao walivamia baadhi ya maduka na kuchoma majengo kadhaa.
Tangu mwanasiasa huyo ajisalimishe gerezani wiki iliyopita, watu sita wamefariki dunia kutokana na ghasia hizo, huku 500 wakiamatwa.
Wafuasi hao waliingia mitaani na kuanza kufanya fujo, mara baada ya kesi ya Zuma kusikilizwa katika Mahakama ya Kikatiba nchini humo, bila mafanikio kwa mwanasiasa huyo, ambaye alitarajia kupewa dhamana au kupunguziwa adhabu yake.
Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, aliwaomba wananchi wasijihusishe na ghasia hizo, huku akiwalaani waliozianzisha.
Zuma alihukumiwa kifungo hicho na Mahakama ya Kikatiba nchini humo, baada ya kubainika na hatia katika kosa la kuidharau mahakama hiyo, kufuatia hatua yake ya kutohudhuria mahakamani kusikiliza kesi ya ufisadi inayomkabili.
Rais huyo wa zamani wa Afrika Kusini, anatuhumiwa kufanya makosa ya ufisadi alipokuwa madarakani, lakini mara kadhaa amekana makosa hayo.
Zuma alikuwa Rais wa Afrika Kusini kwa miaka tisa mfululizo, kuanzia 2009 hadi 2018.
Leave a comment