WANAFUNZI wa ngazi mbalimbali za elimu wametakiwa kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo hapa nchini kwa kuwa kufanya hivyo kunawapa fursa ya kutambua uzuri wa nchi, rasilimali zilizopo na kuwaongezea maarifa na uzalendo kwa nchi yao.
Wito huo umetolewa jana tarehe 9 Julai, 2022 na Mhifadhi na Mkuu wa kitengo cha Utalii, Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, Herman Baltazari alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa Chuo cha Sukari cha Taifa kilichopo Kilombero Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro, wakati walipotembelea Hifadhi ya Taifa ya Mikumi.
Baltazar alisema Hifadhi ya Taifa ya Mikumi imejipanga vyema kupokea watalii wa ndani na nje ya nchi hivyo anawakaribisha watanzania wote hususani wanafunzi kutembelea hifadhi hiyo ambayo inafika kwa urahisi.
Naye Kaimu Mkuu wa Chuo cha Sukari Cha Taifa, Aloyce Kasmir, alisema uongozi na wanafunzi wa chuo hicho wameamua kutembelea hifadhi ya Mikumi kwa lengo la kumuunga Mkono Rais Samia Suluhu Hassan, katika jitihada zake za kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini,lakini pia ni kuwapa fusra wanafunzi wa chuo hicho cha Sukari cha Taifa kutambua vivutio vya utalii vilivyopo nchini.
Mariam Salumu, mwanafunzi wa kozi ya Teknolojia ya uzalishaji wa sukari wa Chuo cha Sukari cha Taifa, akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wa chuo hicho alisema wamefurahishwa na ziara hiyo kwa kuwa wamepata fursa ya kujifunza kuhusu vivutio vya utalii vilivyopo nchini hususani kwenye Hifadhi ya Taifa ya Mikumi hivyo watakuwa walinzi na mabalozi wa kutangaza rasilimali hizo.
Leave a comment