Friday , 26 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa WAMEUMIA 2021; Wengi vigogo CCM, mfumo awamu ya sita umewatema
Habari za SiasaTangulizi

WAMEUMIA 2021; Wengi vigogo CCM, mfumo awamu ya sita umewatema

Spread the love

 

KIBAO kimegeuka juu chini! Ndivyo unavyoweza kuelezea mapito waliyokumbana nayo wanasiasa machachari nchini katika kipindi cha mwaka huu baada ya kuenguliwa katika nafasi zao na mwingine kutupwa ‘lupango’.

Ulikuwa mwaka wa machungu hususani kwa wanasiasa wengi zaidi wa CCM kwa sababu yaliyowatokea mbali ya kuwa ni sawa na anguko la kisiasa lakini pia limewavuruga na wengine kutoamini kutokana na makali ya kisheria waliyokumbana nayo.

Vigogo hao waliokuwa na nyadhifa kubwa serikalini na ndani ya CCM yamkini sasa wanaonja joto la jiwe kutokana na pigo la kuondoka kwa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Magufuli na uongozi mpya wa awamu ya sita ulioingia madarakani ukawatema kwenye mfumo wake.

HUMPHREY POLEPOLE

Kwa sasa ndiye mwanasiasa ambaye moto wake umezidi kuwashwa ndani na nje ya CCM

Polepole ni mwanasiasa aliyetokea kwenye uanaharakati, alipanda wadhifa taratibu baada ya kuteuliwa na Rais wa Awamu Nne, Dk. Jakaya Kikwete kuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba maarufu kama Tume ya Warioba mwaka 2014 kabla ya Rais John Magufuli kumpa cheo cha Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi CCM kisha mbunge wa kuteuliwa.

Awali wakati akila ‘kuku kwa mrija’ kwa vyeo hivyo viwili kwa wakati mmoja chini ya uongozi wa Rais John Magufuli, ulipoingia uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan mara moja aling’oelwa kwenye nafasi moja.

Humphrey Polepole, Aliyekuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM

Aprili 30 mwaka huu, nafasi yake ndani ya CCM ilichukuliwa na Shaka Hamidu Shaka na kubakia na ubunge wa kuteuliwa na rais pekee.

Mambo yalianza kubadilika alipoanza kujitokeza hadharani kupinga chanjo ya Corona na kwenda kinyume na mipango ya Serikali ya Rais Samia ya kwamba watu wachanje.

Polepole pia alipinga mpango wa kuwahamisha wamachinga bila kuwatafutia maeneo rafiki kwa biashara zao jambo ambalo yamkini liliendana sambamba na malengo ya Serikali.

Hata hivyo, kipindi chake cha Shule ya Uongozi ambacho aliendelea kukirusha kwenye televisheni ya Online, Disemba 17 mwaka huu kimepigwa rungu na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) baada ya kusimamishwa kwa muda na kutakiwa kufanyia kazi kasoro mbalimbali ikiwamo kuajiri waandishi na watangazaji wenye uweledi.

Mbali na hilo, tayari Kamati Kuu ya CCM ilimuita na kumhoji huku fununu zikidai ni kupitia kipindi hicho ambacho kinadaiwa kuwa na maudhui yaliyokosoa waziwazi Serikali iliyopo madarakani.

BASHIRU ALLY

Yamkini ndiye mwanasiasa aliyepigwa na ‘kitu kizito kichwani’ baada ya kufariki kwa Rais John Magufuli kwa sababu ndiye aliyemtoa katika nafasi ya uhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam na kumteua kuwa Katibu Mkuu wa CCM nafasi ya juu kabisa ndani ya chama.

Kama hiyo haitoshi, Februari mwaka huu Rais Magufuli alimteua kuwa Balozi na Katibu Mkuu Kiongozi nafasi ya juu kabisa ndani ya Serikali.

Dk. Bashiru Ally

Mwenyezi Mungu alipomchukua Rais Magufuli Machi 17 mwaka huu, Bashiru ambaye alikaa siku 34 tu ndani ya Ikulu, Machi 31 mwaka huu aling’olewa kwenye nafasi hiyo na kuteuliwa kuwa Mbunge. Nafasi yake ilichukuliwa na Balozi Hussein Yahya Katanga.

Ukimya wake, hekima na busara zake yamkini ndizo zinazomfanya asijadiliwe sana ikilinganishwa na vigogo wengine waliong’olewa kwenye nafasi zao huku wakiwa hawaamini kilichowatokea mwaka huu.

LENGAI OLE SABAYA

Waswahili husema kila ‘zama na kitabu chake’, lakini zama hizi kwa kijana mdogo mwenye umri wa miaka 34 pekee, zimekuwa mbaya zaidi maishani mwake baada ya Oktoba 15 mwaka huu kuhukumiwa miaka 30 jela.

Sabaya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai na mwanachama kindakindaki wa CCM, ndiye mkuu wa wilaya wa kwanza kukumbana na adhabu hiyo katika historia ya Taifa hili.

Lengai Ole Sabaya akiwa mahakamani Arusha

Sabaya na wenzake watatu walihukumiwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Arusha, Odira Amworo kifungo cha miaka 30 jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha.

Lengai ambaye alikuwa akimuita Magufuli ‘Baba’

mbali na hukumu hiyo bado ameendelea kuandamwa na mashtaka mazito ambapo sasa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha anaendelea na kesi ya uhujumu uchumi ambayo inamkabili na wenzake sita.

HAMIS KIGWANGALA

Mbunge huyo wa Nzega Vijijini (CCM) ambaye pia alikuwa Waziri wa Maliasili na Utalii katika Serikali ya Awamu ya Tano, mwaka huu hatousahau baada ya kukumbwa na kashfa nzito ya tuhuma za kuiba fedha za Serikali na kujinufaisha binafsi.

Aprili 8, 2021 Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere aliwasilisha ripoti ya mwaka wa fedha 2019/2020 ambapo miongoni mwa Taasisi zilizofanya ubadhirifu wa fedha ni pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii wakati huo Waziri akiwa Hamisi Kigwangala.

Katika ripoti yake CAG alibainisha kuwa Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa (TANAPA) na Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro zilifadhili Tamasha la Upandaji Mlima Kilimanjaro bila kuwepo kwenye bajeti.

Dk. Hamisi Kigwangallah

Ripoti hiyo ilieleza kuwa shindano la ‘Kigwangalla Kili Challenge’ la mwaka 2019 lilitumia Milioni 172 zilizotolewa na TANAPA na Ngorongoro.

Aidha, ripoti ya CAG ilieleza kuwa kituo cha televisheni cha Clouds kililipwa Sh milioni 629.7 na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) kiasi cha Sh milioni 201.4 kwa ajili ya kuonyesha matangazo ya tamasha la urithi lakini hakukuwa na risiti zozote za kielektroniki zilizotolewa kuthibitisha malipo hayo.

Hata hivyo, Kiwagangala alikanusha tuhuma hizo kupitia ukurasa wake wa Twitter kwa kuandika hivi “Mimi sintosema chochote, nimemuachia Mungu apigane kwa niaba yangu. Nakubali ‘kuwajibika kisiasa’, siwezi kuwakana wasaidizi wangu, lakini sikuiba pesa wala kufaidika ‘binafsi’ kwa namna yoyote ile, lakini pia mimi sikuwa ‘afisa masuuli’ na hivyo sikuhusika na kuidhinisha pesa.

ASKOFU GWAJIMA, JERRY SILAA

Licha ya wabunge hao wa CCM kutofautiana kimtizamo kuhusu mambo mbalimbali, lakini walikumbwa na hatia moja ya kutoa kauli zilizoshusha hadi na heshima ya Bunge.

Agosti 31 mwaka huu Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ilitoa azimio la kuwasimamisha mikutano miwili wabunge hao Askofu Josephat Gwajima (mbunge Kawe) na Jery Silaa (mbunge Ukonga)kwa kuwatia hatiani.

Gwajima ambaye ni Askofu wa madhehebu ya kanisa la uzima na ufufuo amekuwa akitoa kauli zinazokinzana na msimamo wa chama chake na serikali hususani katika suala zima la chanjo ya Covid 19.

Askofu Josephat Gwajima na Jerry Silaa wakisubiri kuhojiwa na Kamati ya Maadili ya Wabunge wa CCM

Gwajima amekuwa akisema kuwa yeye na waumini wa kanisa lake hawatochanjwa chanjo hiyo hadi hapo wizara ya afya itakapotoa elimu na ufafanuzi wa kina kuhusiana na madhara ya chanjo hiyo.

Aidha, Jerry Silaa naye alidaiwa kusema uongo kwamba mishahara ya Wabunge haikatwi kodi hivyo Bunge likaazimia Silaa na Gwajima kutoahudhuria mikutano miwili mfululizo na kuondolewa kwenye uwakilishi wa Bunge la Afrika.

ALBERT CHALAMILA

Juni 11 Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania atengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Albert Chalamila na hivyo kumfanya kada huyo kindakindaki wa CCM kuwa mkuu wa mkoa wa kwanza kutenguliwa chini ya utawala wake.

Licha ya kwamba hapakuwa na taarifa rasmi kuhusu sababu za kuenguliwa katika nafasi hiyo, Chalamila ambaye alikuwa Mwenyekiti wa CCM Iringa, mwaka 2018 aliteuliwa na Rais Magufuli kuwa mkuu wa mkoa Mbeya. Alikuwa ni mkuu wa mkoa mwenye machachari.

FREEMAN MBOWE

Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema, ni mmoja wa viongozi wa upinzani walioonja machungu katika mwaka huu wa 2021 baada ya kukumbwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka sita ikiwamo ugaidi.

Mbowe na wenzake watatu, alikamatwa Juni mwaka huu na kufikishwa mahakamani Agosti mwaka huu, hadi sasa yupo mahabusu Ukonga huku kesi yao ikiahirishwa hadi Januari 10 mwaka 2022.

KAULI ZA WACHAMBUZI

Akizungumzia mapito waliyopitia wanasiasa hao, pamoja na wengine, Mshauri Mkuu wa Taasisi ya Ufuatiliaji wa masuala ya Bunge, Dk. Marcus Albanie alisema machungu hayo yametokana na hali ya kisiasa iliyochipuka miaka mitano iliyopita.

Amefafanua kuwa katika miaka mitano iliyopita chini ya utawala wa Rais Magufuli, palijitokeza makundi matatu yaliyojipambanua kutonyamaza kimya kuhusu ukandamiza wowote wa haki za binadamu, kundi la waliojiunga na utawala uliokuwepo na kundi la tatu ni lilela waliokwenda chini ya udongo kwa maana ya kwamba kuficha makucha yao.

Amesema baada ya utawala wa awamu ya tano kufutika, ndipo athari za matokeo ya makundi hayo zimejitokeza kwa maana kuwa wale walioamua kutonyamaza katika uvunjwaji wa haki za binadamu wamekumbwa na kesi kama ilivyo kwa Mbowe.

Wale waliokuwa katika kundi la utawala, wamekumbwa na kesi za ukiukwaji wa sheria kama ilivyo kwa Sabaya wakati kundi la mwisho lililokuwa limeficha makucha sasa ndio limeanza kujitokeza.

Alisema kutokana na mabadiliko ni dhahiri mwaka 2022 wanasiasa wanapaswa kujifunza kuenenda na wakati ili wasikumbane na machungu kama ya mwaka huu.

Hoja hizo ziliungwa mkono na Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma wa CUF- Mohamed Ngulangwa ambaye alisisitiza wanasiasa hao walioonja machungu ambao wengi wao wanatoka chama tawala CCM, wanavuna walichokipanda.

Alisema machungu hayo wanayopitia hususani wanasiasa wa CCM mwaka huu yanapaswa kuwafunza wanasiasa wajao kuwa cheo ni dhama au ni kama koti la kuazima.

Aidha, aliongeza kuwa machungu yanayowapata wanasiasa wa upinzani sasa yanatokana na mfumo mbovu wa demokrasia hivyo ni vema wanasiasa kuungana kupigania mabadiliko ya kimfumo.

Imendaliwa na Gabriel Mushi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

error: Content is protected !!