Thursday , 25 April 2024
Home Habari Mchanganyiko ACT- Wazalendo yaitaka Serikali kuingilia kati bei ya mbolea
Habari Mchanganyiko

ACT- Wazalendo yaitaka Serikali kuingilia kati bei ya mbolea

Spread the love

 

CHAMA cha siasa cha upinzani nchini Tanzania cha ACT-Wazalendo, kimeitaka Serikali ya nchi hiyo kuingilia haraka na kudhibiti kupanda kwa kasi isiyo ya kawaida kwa bei ya mbolea. Anaripoti Victoria Mwakisimba, TUDARCo … (endelea).

Taarifa iliyotolewa kwa umma chama hicho, imemnukuu Katibu Mkuu wake, Ado Shaibu akizungumza na viongozi na wanachama wa jimbo la Songea Mjini mkoani Ruvuma jana Jumatano, tarehe 22 Desemba 2021, akisema iwapo Serikali haitachukua hatua za muda mfupi, wa kati na mrefu kwenye suala hilo wakulima wa Tanzania wataathirika sana.

Alizungumzia hilo baada ya kupokea kero mbalimbali kutoka kwa wanachama na viongozi, Ado alisema bei ya mbolea imepanda kwa kasi Songea.

Mathalani, mbolea aina ya Urea iliyouzwa Sh.52,000 msimu uliopita, sasa inauzwa Sh. 105,000 kwa mfuko hali inayowafanya wakulima kushindwa kumudu kununua. Hali ipo hivyohivyo kwenye aina zote za mbolea.

Ado alisema ACT Wazalendo haijaridhishwa na majibu ambayo Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda na naibu wake, Hussein Bashe wameyatoa kuhusiana na suala la mbolea.

Ado Shaibu, Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo akizungumza na wanachana wa chama hicho katika jimbo la Nyasa mkoani Ruvuma.

“Ndugu yangu Bashe alifika hapa Songea. Akazungumza na wadau wa kilimo, Profesa Mkenda alifika pia, kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya mbolea duniani,” alisema

“Hawakuja na majawabu, walikuja na malalamiko. Kwamba bei ya soko la dunia na ugonjwa wa Korona ndio vimesababisha kupanda kwa bei ya mbolea. Hakuna hatua za maana za dharura walizosema” alisema Ado

Katibu mkuu huyo alisema, “tunatoa rai kwa Rais Samia Suluhu Hassan, aingilie upesi suala la mbolea na kuchukua hatua za upesi. Mosi, Serikali itoe ruzuku ili kushusha bei ya mbolea.”

Alisema, sehemu ya fedha za mkopo wa Korona kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) itumike kugharamia hili. Pili, katika msimu huu wa kilimo, Serikali ipunguze au iondoshe ushuru wa kuagiza mbolea nje ili kushusha bei.

Tatu, katika hatua za muda mrefu, Serikali iwe na mkakati wa kuimarisha uzalishaji wa mbolea nchini. Hivi sasa, viwanda vya ndani vinazalisha asilimia 5 tu ya mahitaji ya ndani. Kwenye Mkakati huo, Serikali iweke vichocheo (incentives) vya kuwavutia wawekezaji kwenye sekta ya viwanda vya mbolea”.

Prof Adolf Mkenda, Waziri wa Kilimo

Ado alisema wakulima wamekuwa wakijitahidi kuongeza uzalishaji licha ya kutumia zana duni, kupanda kwa bei ya pembejeo na kuporomoka kwa bei ya mazao.

“Takwimu za NBS za mwezi Juni 2021 zinaonesha uzalishaji wa mazao ya nafaka nchini uliongezeka kutoka tani 16,293,637 mwaka 2019 hadi tani 18,196,733 mwaka 2020. Iwapo hatua za upesi hazitachukuliwa kushusha bei ya mbolea, uzalishaji wa mazao utashuka maradufu” alisisitiza.

Ado akiambatana na naibu katibu mwenezi wa chama hicho, Janeth Rithe, katibu wa sera na utafiti, Idrisa Kweweta na naibu katibu mwenezi wa ngome ya vijana, Antony Ishika anaendelea na ziara ya Sekretarieti ya chama kwenye mikoa ya Ruvuma, Mkoa wa kichama Selous, Lindi, Mtwara, Pwani na Tanga.

Lengo la ziara hiyo ni ujenzi wa chama, kuhamasisha michango ya mkutano mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 Januari 2022 na kuelezea mageuzi ya uendeshaji chama kisayansi yanayotarajiwa kuzinduliwa kwenye mkutano huo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Wakili: Ukimpa zawadi mwenza marufuku kumpora hata mkiachana

Spread the love  WANANDOA na watu waliko kwenye mahusiano ya kimapenzi, wamekumbushwa...

Habari Mchanganyiko

Majaliwa: Mvua zimesababisha vifo vya watu 155, kuendelea hadi Mei

Spread the love  WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema mvua kubwa za El-Nino...

Habari Mchanganyiko

Exim Bank yatoa  vitanda kwa shule ya Jeshi la Polisi Moshi

Spread the love  BENKI ya Exim imekabidhii  seti ya vitanda kwa Shule...

Habari Mchanganyiko

NBC yakabidhi vitanda Shule ya Polisi Moshi

Spread the loveBenki ya NBC imekabidhi msaada wa vitanda 28 kwa Shule...

error: Content is protected !!