October 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mwanafunzi afa kwa kukabwa na mkate, soda

Spread the love

 

SHEREHE za kumpata mshindi wa kula mkate na kunywa soda jana tarehe 22 Disemba, 2021 ziliisha kwa simanzi, baada ya mwanafunzi mmoja kukabwa na mlo huo hadi kufa katika Shule ya msingi ya Sikura, Kaunti ya Busia nchini Kenya. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Marehemu Harrison Oduor Ouma, alikuwa kati ya wanafunzi waliojawa na furaha akitumaini kuwa angeshinda na kutuzwa ila chakula hicho kiilishia kukwama kooni na kwa masikitiko makubwa, kilisababisha mauti yake.

Shindano hilo liliidhinishwa na usimamizi wa shule hiyo.

Juhudi za walimu na wanafunzi wenzake kumpa huduma za kwanza hazikufanikiwa kwa kuwa alifariki wakati akikimbizwa hospitalini.

“Alikabwa na kipande cha mkate ambacho kilikwama kwenye koo lake kisha akapoteza fahamu licha ya kupatiwa huduma ya kwanza na walimu pamoja na wanafunzi wenzake.

“Uongozi wa shule hiyo ulihakikisha kuwa anakimbizwa hospitalini lakini kwa masikitiko makubwa, akafariki kabla ya kufika katika zahanati ya Buluani, mita chache kutoka shule hiyo,” alisema Mkuu wa Polisi wa Kaunti ndogo ya Butula, Jacob Chelimo.

Wanafunzi walikuwa wakishiriki mashindano hayo ya kula mkate na kunywa soda siku ya mwisho wa muhula huu kabla ya kuenda likizo ya sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya.

Chelimo alithibitisha kuwa Mwalimu Mkuu, Peter Tetela alipiga simu na kumwaarifu kuwa mvulana huyo alikabwa na mkate huo hadi akafariki shuleni humo.

Mtaalamu wa masuala ya kimatibabu Dk. Donald Musi amezishauri shule kuepuka tabia ya kuwaruhusu wanafunzi kushiriki mashindano ya kula chakula hasa mikate akisema ni hatari na yanaweza kusababisha vifo.

Pia amependekeza kuwa iwapo lazima mashindano hayo yafanyike, basi vitumike vyakula ambavyo ni vyepesi na haviwezi kumkaba mtu.

Mwili wa mwanafunzi huyo umehifadhiwa katika mochwari ya Sega.

error: Content is protected !!