Friday , 26 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Vyama 11 vya siasa Tanzania vyataka uchaguzi usogezwe mbele
Habari za SiasaTangulizi

Vyama 11 vya siasa Tanzania vyataka uchaguzi usogezwe mbele

Sanduku la kura
Spread the love

JANGA la mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu, inayosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19), limeathiri shughuli za vyama vya siasa katika maandalizi ya kuelekea uchaguzi mkuu wa 25 Oktoba mwaka huu. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Tangu mgonjwa wa kwanza alipobainika nchini humo tarehe 16 Machi 2020, serikali imepiga marufuku mikusanyiko isiyokuwa ya lazima ikiwamo ya kisiasa, ili kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo.

Wakati tahadhari ikiendelea kusisitizwa ili kuepuka kuenea kwa ugonjwa huo, baadhi ya vyama vya siasa vilivyozungumza na MwanaHALISI ONLINE vimeeleza jinsi Corona inavyoathiri maandalizi vyama hivyo, kuelekea uchaguzi ujao.

Wamesema, kipindi kama hiki, vikao mbalimbali vya kujadili jinsi ya kupata wagombea vingekuwa vimeanza lakini kwa sasa hilo haliwezekani zaidi ya kupata wagombea.

Mkuu wa Idara ya mahusiano ya umma ya NCCR-Mageuzi, Edward Sembeye, amedai kuwa Corona imesababisha chama hicho kutopata wagombea wazuri na wanaohitajika na wananchi.

Amesema, kuwapo kwa ugonjwa huo, kumesababisha kushindwa kufikia katika maeneo kadhaa nchini ili kujua kama wana sifa na wanakubalika.

Edward Sembeye, Mkuu wa Mawasiliamo ya Umma NCCR-Mageuzi

Amesema, “Corona imeathiri kwa kiasi kikubwa mkakati wetu wa kupata wagombea. Kuwapo kwa ugonjwa huu, kunatufanya tushindwe kuwafikia wapigakura.

“Lakini linaporudi kwenye itikadi yetu ya UTU bado licha ya kwamba tulipaswa kupiga hatua kwenye maandalizi ya uchaguzi kwa wagombea kujitangaza, bado tunathamini uhai wa binadamu wenzetu,” ameeleza.

Alipoulizwa nini kifanyike kutokana na athari hizo, Sembeye amesema, NCCR-Mageuzi haiwezi kushauri chochote, kwa kuwa hadi sasa serikali haijatoa msimamo juu ya namna uchaguzi huo utakavyofanyika.

“Tuangalie njia sahihi zitakazotusaidia kwenda kwenye uchaguzi bila kuleta madhara, kwa sasa nachelea kusema chochote naamini mamlaka zinajadiliana namna gani tutaelekea kwenye uchaguzi. Huwezi kushauri jambo ambalo halijatolewa taratibu,” ameeleza.

Naye Janeth Rithe, Naibu Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama cha ACT-Wazalendo, ameliambia MwanaHALISI ONLINE kuwa janga la Corona limeathiri shughuli za maandalizi ya chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu ujao, hususan kushindwa kufanya mikutano.

Rithe amesema, chama chake kama vilivyo vyama vingine, kinashindwa kuwafikia wanachama pamoja na viongozi wake, kutokana na asilimia kubwa ya viongozi na wanachama wake walioko maeneo ya vijijini, kutokuwa na uwezo wa kushiriki shughuli za mtandaoni.

Zitto Kabwe, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo

“Corona imetuathiri katika maandalizi ya chama kwa ajili ya kushiriki uchaguzi, lakini inabidi tuangalie namna ya kukabiliana na changamoto hiyo, ili kuhakikisha shughuli zetu haziathiri afya za wananchi,” amesema.

Kwa upande wake, Mhandisi Mohammed Ngulangwa, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano wa Chama cha Wananchi (CUF) amesema, Covid-19, imekwamisha mchakato wa upatikanaji wagombea hasa wa nafasi ya urais, ubunge, udiwani na uwakilishi kwa upande wa Zanzibar.

Ametaka serikali kuangalia namna bora itakayosaidia kupunguza makali ya athari ya ugonjwa wa Corona.

Amesema, “wengi wamejitokeza kutangaza nia ya kugombea, lakini Corona imesababisha tukose fursa ya kufanya mkutano wa kuwateuwa, sababu mikusanyiko imekatazwa, pia sio watu wote kwa kuzingatia hadhi zao wanaweza kutangaza nia za kugombea katika mitandao ya kijamii.”

Eugine Kabendera, Naibu Katibu Mkuu CHAUMA, yeye ameishauri serikali isogeze mbele uchaguzi huo, ili kutoa nafasi kwa vyama vya siasa kujiandaa vizuri zaidi na kuwakinga wananchi na Corona.

“Tungetamani kuona uchaguzi ungesogezwa mbele ili kuwapa watu nafasi ya kutibu hili gonjwa, suala la uchaguzi linahitaji watu wawe na afya, na wawe na uwezo wa kuamua, “ameeleza Kabendera.

Hashim Rungwe, Mwenyekiti wa Chama cha Umma

Mwanasiasa huyo amesema, kutokana na athari za janga la Corona, vyama vinashindwa kuandaa baadhi ya shughuli zake, hivyo kama uchaguzi huo utafanyika kama ulivyopangwa, havitaweza kushiriki kwa ufanisi.

“Tulipanga tufanye mikutano ya ndani kwa maana ya kamati kuu na halmashauri kuu ambayo maamuzi yangetupelekea kuona namna gani ya kupata wagombea,” amesema Kabendera na kuongeza: “Lakini tumeshindwa kufanya hivyo, kwa sababu nchi ni kubwa.

“Hatuwezi kuteua wagombea, bila kupata maoni ya wananchi kwa kufanya mikutano ya hadhara au ya ndani,” ameeleza Kabendera.

Abdul Mluya, Kiongozi wa Umoja wa Vyama 10 visivyokuwa na Uwakilishi bungeni amesema, Corona limesababisha vyama hivyo kushindwa kukutana, ili kujadili namna ya kushiriki uchaguzi huo.

Kwa mujibu wa Mluya, “Corona imekuwa na athari kwa sababu hata kama ukitaka kujipanga kuingia kwenye uchaguzi, maana yake lazima uwe na mikusanyiko midogo ya ndani na ya wanachama. Uzingatia maelekezo ya Serikali imetuwia vigumu kufanya hivyo, maana yake shughuli za kuandaa wagombea zimesimama.”

Amesema, “kwenye umoja wetu hatujakutana tangu janga hili limeanza, ilikuwa desturi yetu tukutane kuangalia kwenye uchaguzi tunaingiaje.”

Mluya ameishauri Serikali kusogeza mbele uchaguzi huo, ili vyama vipate nafasi ya kujiandaa.

“Janga la Corona ni la dunia, sio la nchi na kama ni la dunia lina muingiliano mkubwa sana. kama juhudi za mataifa makubwa zinaonekana kufeli, tutaingiaje kwenye uchaguzi unaohusisha mikusanyiko ya watu, ndio maana tukashauri zoezi la uchaguzi lisimame, ” amesema Mluya.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

error: Content is protected !!