KATIKA kuadhimisha wiki ya sheria nchini, Mahakama ya Wilaya Ulanga imetoa elimu ya sheria kwa wadau mbalimbali kwa lengo la kuwaelimisha kuhusu masuala ya maadili na malezi bora kwa watoto. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).
Akizungumza katika kilele cha Siku ya Sheria nchini wilaya ya Ulanga leo Alhamisi, Hakimu Mkazi Mfawidhi mahakama ya wilaya hiyo, Christopher Bwakila amesema katika kutoa elimu hiyo, watumishi wa mahakama hiyo na wadau wake walijigawa katika makundi matatu.
“Tulitembelea shule za Sekondari (mfano Kwiro Boys, Lupiro, Celina Kombani, Mwaya, Nawenge): Shule za msingi (Mahenge A na Mahenge B) ambapo kamati ya uelimishaji ilifanikiwa kufanya mkutano na wazazi wa wanafunzi wanaosoma katika shule hizo kwa lengo la kuwaelimisha kuhusu masuala mbalimbali yakiwemo masuala ya maadili na malezi bora kwa watoto.
“Pia tulifanya mikutano maeneo mbalimbali yenye mikusanyiko kama vile Soko la Lupiro na Mahenge, Mawasiliano, Safari Road, Mwaya Center, Ilonga, Chikuti, Idunda, kwenye vituo vya bodaboda (Hospitali ya Wilaya Ulanga, Togo, Stone na Stendi),” amesema.
Aidha, amesema kwa niaba ya kamati iliyohusika na utoaji elimu na Mahakama kwa ujumla amemshukuru Mratibu Elimu Kata ya Mahenge Mjini pamoja na Wakuu wa Shule za Msingi na Sekondari ambazo kamati ya elimu ilitembelea na kuendesha mkutano.
“Bila kuwasahau viongozi wote wa Kata na Vijiji ambao kamati ilitembelea maeneo yao na kufanya mikutano ya utoaji elimu ambapo walitusaidia kuwataarifu wananchi kuhusu ujio wetu,” amesema.
Ameongeza kuwa mahakama ya Tanzania imekuwa ikiadhimisha wiki na siku ya sheria kila mwanzoni mwa mwaka na mwaka huu wa 2024, kuanzia tarehe 24 Januari 2024 hadi 30 Januari 2024 wananchi walipata elimu kuhusu masuala mbalimbali ya kisheria.
Amesema ana imani kuwa elimu waliyoitoa wakati wa wiki ya sheria itawasaidia sana wananchi kwa sababu wananchi wengi walionyesha kuridhika na elimu iliyotolewa na kutamani utoaji wa elimu uwe endelevu.
“Napenda kuwahakikishia elimu hii itakuwa endelevu kwakuwa itakuwa inatolewa Mahakamani asubuhi kabla ya kuanza shughuli za Mahakama.
“Leo tunafikia kilele cha siku ya sheria nchini ambapo maadhimisho ya mwaka huu, yanaongozwa na kauli mbiu isemayo. “Umuhimu wa dhana ya haki kwa ustawi wa taifa: nafasi ya mahakama na wadau katika kuboresha mfumo jumuishi wa haki jinai”.
Amesema kauli mbiu ya mwaka huu kwenye siku na wiki ya sheria imekuja katika kipindi sahihi kwa sababu kwa sasa Mahakama ya Tanzania inatekeleza Mpango Mkakati wa miaka mitano wa awamu ya pili (2020/21- 2024/25) ambapo kuna maboresho mbalimbali.
“Maboresho hayo yanaendelea kutekelezwa na Mahakama ili kuendana na nguzo tatu za mpango mkakati huo ambazo nitazielezea katika hotuba hii. Lengo kuu la kutekeleza Mpango Mkakati huu ni kuhakikisha Mahakama ya Tanzania inafikia lengo lake kuu ambalo ni utoaji wa haki kwa wakati na kwa watu wote,” amesema.
Leave a comment