TUME ya Madini imewataka wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu mkoani Geita kuzingatia sheria ya mazingira na afya migodini.
Pia imetoa wito kwa watu wote wanaowekeza katika sekta ya madini wajikinge na walinde mazingira kwenye maeneo wanakochimba Madini hayo. Anaripoti Paul Kayanda, Geita… (endelea).
Hatua hiyo ni kujikinga na vihatarishi vinavyowazunguka katika maeneo yao ya kazi ili wachimbe katika hali ya usalama zaidi na kufaidi kile wanachokipata.
Hayo yameelezwa leo tarehe 29 Septemba, 2022 na Afisa mazingira kutoka Tume ya Madini, Hyasinta Laurean katika maonesho ya tano ya kitaifa ya Teknolojia ya Madini 2022 yanayoendelea katika viwanja vya Bombambili mkoani hapa.
“Tupo hapa kutoa elimu kwa Watanzania ili wajue Tume ya Madini inafanya nini, kwa upande wangu naweza kuelezea machache juu ya mazingira na Afya Migodini nawaelezea Watanzania wanaowekeza katika Madini,” amesema Laurean na kuongeza.
“Wanatakiwa wajikinge na walinde mazingira yao yaliyowazunguka na maeneo wanayoyachimba madini hayo kwa mfano kama hapa tuna vifaa vya kujikinga wachimbaji pale wanapokuwa wanachimba ama wanapokuwa wanachenjua dhahabu ili kujizuia na vihatarishi vilivyopo katika maeneo yao ya kazi,” amesema.
Aidha, Afisa huyo amewataka kuchimba katika hali ya usalama katika maeneo yao ya uchimbaji hatua ambayo watanufaika na kile watakachokipata kwenye shughuli hiyo vile vile kuwalinda na kuwanufaisha watanzania wenzake ambao wapo pembeni.
Kwa upande wake Meneja Habari na Mawasiliano Tume ya Madini, Greyson Mwase ametumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wakazi wa Mkoa wa Geita pamoja na Mikoa jirani ya Mwanza, Shinyanga na Kagera kufika kwenye maonesho hayo na kutembelea banda la Tume ili kupata huduma mbalimbali.
Leave a comment