April 12, 2021

Uhuru hauna Mipaka

TRC yatakiwa kusafirisha mbolea kwa wingi

Treni ya Shirika la Reli Tanzania (TRC)

Spread the love

SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC), limetakiwa kutoa kipaumbele cha kusafirisha mbolea nyingi kwa wakati mmoja na kwa gharama nafuu ili kumfikia mkulima kwa wakati na bei nafuu. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 10 Mei 2019 bungeni na Naibu Waziri wa Kilimo, Omari Mgumba alipojibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Taska Mbogo (CCM).

Katika swali lake, Mbogo alidai kwamba, Mkoa wa Katavi unapata mvua za masika kuanzia Septemba na Oktoba, lakini mara nyingi pembejeo zimekuwa zikichelewa kupelekwa wakati mwingine hadi Novemba.

“Je, serikali ina mpango gani wa kupeleka kwa wakati pembejeo mkoani Katavi,” ameuliza Mbogo.

Akijibu, Mgumba amesema serikali  imelielekeza Shirika la Reli Tanzania kutoa kipaumbele cha kusafirisha mbolea nyingi kwa wakati mmoja na gharama nafuu ili kumfikia mkulima kwa wakati na bei nafuu.

Amesema, serikali inakusanya mahitaji ya mbegu bora na viutilifu kutoka katika mikoa, ili kuhamasisha kampuni na wafanyabiashara kupeleka pembejeo kwa wakulima kabla ya msimu wa kilimo kuanza na wakati wa mauzo ya mazao.

“Vile vile ziada ya mbolea iliyopo nchini inaendelea kusambazwa katika maeneo mbalimbali kulingana na msimu ambapo hadi tarehe 30 Machi 2019, kulikuwa na tani 147,913 za mbolea,” amesema.

error: Content is protected !!