December 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

TFS yakutanisha wadau kujadili urejeshaji uoto wa asili

Spread the love

 

WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imekutanisha wadau mbalimbali kujadili mpango wa urejeshaji uoto wa asili barani Afrika (AFRI100) unaolenga kurejesha hekta milioni 100. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Warsha hiyo inayofanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam ni mwendelezo wa mikakati ya taasisi hiyo katika kutekeleza ahadi ya Tanzania ya kurejesha hekta milioni 5.2 katika kusaidia kufikia lengo la hekta milioni 100 barani Afrika na hekta milioni 350 duniani kufikia mwaka 2030.

Akifungua warsa hiyo leo Jumanne tarehe 22, Novemba, 2022, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Marry Masanja, ameipongeza TFS kwa kuandaa warsa ya kujadili namna ya kupambania kurudisha uoto wa asili.

Ili kufikia lengo la Tanzania, Masanya ameagiza kuwepo kwa mabalozi wa mazingira kila mkoa watakaosaidia kutoa mrejesho wa utekelezaji wa mikakati itakayowekwa ya upandaji miti na kuokoa maeneo yaliyovamiwa na wananchi.

Pia ameagiza mikoa yote nchini kuwa na kampeni ya kijani baada ya kuona mafanikio makubwa katika kampeni ya Dodoma ya kijani.

“Naelekeza kampeni isiwe Dodoma ya kijani pekee, kila mkoa uwe na kampeni yake ya kuhakikisha mkoa unakuwa wa kijani kwa kupanda miti na kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira,” amesema Masanja.

Kwa upande wake Kamishna Mhifadhi wa TFS, Profesa Dos Santos Silayo, alisema katika kufikia lengo la Tanzania taasisi hiyo imejipanga kuhakikisha maeneo yaliharibiwa na yale yasiyo na miti yanapandwa miti ili kuongeza wigo wa maeneo yenye miti.

Amesema TFS inashirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Misitu (TAFORI) katika kuhakikisha wanatambua ni miti gani ya kupanda inayoendana na mazingira husika.

“Tunataka kurejesha uoto na kuzuia maeneo ya misitu yanayotaka kuharibika ikiwa hatutachukua hatua na tunafanya shughuli mbalimbali, moja ni kuhakikisa ameneo ambayo yana uoto hayaharibiwi na yale yaliyoharibiwa yanarejeshewa uoto wake,” amesema Profesa Silayo.

Amesema mkakati huo si tu unalenga kuboresha mazingira yaliyoharibika bali pia kuhakikisha jamii zinazoishi maeneo mbalimbali na kutegemea mazingira katika maisha yao zinaimarika kiuchumi ili ziachane na shughuli zinazoharibu mazingira kama vile uchomaji wa mkaa na ukataji kuni.

“Jamii masikini hutegemea zaidi mazingira yao kuishi kwahiyo kunyanyua uwezo wa wananchi kwa kuboresha maisha yao kama kupeleka nishati mbadala, shule, afya na maji vinachangia kuhakikisha misitu haiharibiki,” amesema.

Amesema lengo la kukutana ni kuweka msingi wa namna ya kukusanya rasilimali fedha, kuangalia uwezo wa rasilimali watu na kiteknolojia na kuweka msingi wa namna ya kufuatilia na kutoa taarifa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TAFORI, Dk. Revocatus Mshumbusi, amesema taasisi hiyo inashirikiana na TFS katika kutafiti ni miti gani inafaa kupanda sehemu gani.

“Si kila mti unaweza kuota sehemu yeyote, kwahiyo kazi yetu ni kutafiti udogo kujua unaendana na miti gani,” amesema Dk. Mshumbusi.

Amesema kwa utafiti waliofanya unaonesha kuwa karibu hekta 400,000 za uoto wa asili zimeharibiwa ambapo amebainisha sababu kuu mbili ikiwemo shughuli za kibinadamu na mabadiliko ya tabia ya nchi.

error: Content is protected !!