CHAMA cha Mabenki Tanzania (TBA) kimetoa wito kwa taasisi za kifedha nchini kuhakikisha kuwa makundi yote kwenye jamii hususani wanawake ushirikishwaji wao unapewa kipaumbele. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).

Akizungumza katika hafla ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani iliyofanyika jana tarehe 16Machi 2023 jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chama cha Mabenki Tanzania (TBA) ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya Taifa (NBC), Theobald Sabi alisema ni muhimu kwa taasisi za kifedha kuhakikisha kunakuwa na ushirikishwaji wa wanawake kwenye huduma za kibenki au kifedha nchini.
“Tunatambua kuwa wanawake ni sehemu kubwa ya jamii yetu, zaidi ya asilimia 51 ya watanzania wote ni wanawake na kwa hivyo ni muhimu tunapoongeza ujumuishwaji wa kifedha kwenye jamii kundi la wanawake lisiachwe nyuma,” amesema Sabi.

Sabi amebainisha kuwa kwa upande wa benki ya NBC wameanza na wafanyakazi wakijaribu kuhakikisha kuwa kama benki wanakuwa na sera rafiki kwa wanawake ili waweze kufikia malengo yao ya kikazi, kiajira, na kiuchumi.
Aidha naye Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Mabenki Tanzania (TBA), Tusekelege Joune amesema inatia hamasa kuona kuwa benki nyingi nchini zimekuwa mstari wa mbele kubuni bidhaa mbalimbali ambazo zimekuwa maalum katika kukidhi mahitaji ya wanawake nchini.

“Tunashukuru kuwa benki zimekuwa mstari wa mbele katika kuja na bidhaa mbalimbali ambazo zimekuwa mahsusi kwa ajili ya wanawake nchini ikiwamo wafanyabiashara, akihitaji huduma za kibenki anakutana na bidhaa ambayo imeandaliwa kwa ajili ya kukidhi mahitaji yake,” amesema Joune.
Joune ameongeza kuwa maadhimisho hayo ya Siku ya Wanawake Duniani kwa upande wa sekta ya kibenki kumekua na ongezeko kwa benki kuja na huduma ya dhamana maalum kwa ajili ya wanawake.
Pia kumetolewa hati fungani kwa ajili ya maendeleo ya wanawake ikiwa ni jitihada mbalimbali zinazofanywa na sekta hiyo katika kuinua wanawake.
Leave a comment