December 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Stori ya Enock iliyomuumiza Lissu Singida

Spread the love

STORI ya kushambuliwa kwa Wilfred Enock, mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), imemuumiza Tundu Lissu, mgombea urais wa Tanzania kupitia chama hicho. Anaripoti Mwandishi Wetu, Singida … (endelea).

Leo Jumatatu tarehe 12 Oktoba 2020, Lissu alifika nyumbani kwa Enock kumjulia hali baada ya kushambuliwa kwa madai ya kupeperusha bendera ya chama hicho.

Akizungumza na Lissu kuhusu mkasa huo, Enock amemweleza kwamba tukio hilo lilitokea tarehe 8 Oktoba 2020 ambapo alikuwa njiani kurejea nyumbani kwake.

Amesema, alipokuwa njiani akirejea nyumbani kwake, aliona watu watatu wakimfuata kwa nyuma na pale alipojaribu kuongeza kasi ya kutembea na wao waliongeza kasi kumfuata.

Na pale walipomfikia, walimpiga mtama na kuanguka chini “wakati nakata kona kwenye mtaro, wakanipiga mtama, wakati naanguka chini, nilitanguliza mikono ili kichwa kisigonge ukuta.”

Wilfred Enock

“Nikaanguka chini, sasa huyu mwingine ndio akaja na kisu akaja akanitoboa (anaonesha eneo la shingo). Nikauliza mna kisa na mimi, akasema unajifanya mjanja na hii bendera ya Chadema.”

Wakati anasimulia tukio hilo,  Enock alikuwa akivua fulana yake ili kumuonesha Lissu na timu yake majeraha aliyoyapata kutokana na kisago kutoka kwa watu hao.

Lissu alimuuliza kama alitumia dawa ya maumivu baada ya kushambuliwa ambapo Enock alijibu, amepaka na kwamba, dawa hiyo yenye thamani ya Sh. 40,000 ilikuwa ni mkopo ambapo tayari amelipa Sh.5,000 na anadaiwa Sh.35,000.

Licha ya kuahidi kulipa deni hilo kwa kumpa fedha, Lissu amempa pole kijana huyo akimwambia “haya ndio mambo tunayopigania.”

Huku akitoa bendera nyingine ili amkabidhi, Lissu alikuwa akisema “si bendera inawakera, sasa nimekupa kubwa yake. Hii ndio kiboko yao. Utafute mti mrefu zaidi halafu unaifungia juu zaidi ili waione wakiwa kilomota 10.”

Baada ya kukutana na  Enock, Lissu aliendelea na safari yake ambapo wakazi wa wa Kijiji cha Tumuli mkoani Singida, walizingira barabara ambayo Lissu alikuwa akipita.

Tukio hilo limetokea leo wakati Lissu ambaye pia ni makamu mwenyekiti wa chama hicho, akielekea baadhi za Wilaya za Singida, Tabora na Shinyanga kwa ajili ya mikutano ya kampeni.

Alipofika eneo la Tumuli, Lissu alikuta kundi kubwa la watu wakiwa na pikipiki, mabango, bendera na nguzo zinazofanana na rangi ya chama hicho wakiwa wamesimama kwenye barabara.

Wananchi hao walijipanga kwenye eneo hilo kwa lengo la kuzuia msafara kupita eneo hilo bila kusimama. hata hivyo, Licha ya Lissu kutakiwa kusimama eneo alilokusudia kufanya mkutano kwa mujibu wa polisi, alilazimika kusimama na kusalimia wakazi waliokuwa wakimsubiri.

error: Content is protected !!