May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

SMZ, LSF wazindua wiki ya msaada wa kisheria

Spread the love

 

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), kwa kushirikiana na Shirika linaloshughulika na masuala ya kisheria ‘Legal Services Facility (LSF)’, imezindua wiki ya msaada wa kisheria visiwani humo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Uzinduzi huo umefanyika leo Jumatatu, tarehe 7 Juni 2021, visiwani Zanzibar, huku mgeni rasmi akiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora wa SMZ, Haroun Ali Suleiman.

Akizindua zoezi hilo, linalotarajiwa kufika tamati tarehe 12 Juni 2021, Suleimani amesema litasaidia kupanua wigo wa utoaji msaada wa kisheria, kwa wananchi wote hususan wanawake.

“Kwa muda mrefu serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali, zinazolenga kujenga ustawi wa haki za wanawake na watoto nchini,”

“Mathalani, tumeanzisha mahakama ya udhalilishaji ili kuangalia masuala ya udhalilishaji kwa watoto na wanawake, kisha kutoa adhabu zinazostahili kwa watuhumiwa,” amesema Suleiman.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa LSF, Lulu Ng’wanakilala, amesema taasisi yake imedhamini zoezi hilo, ili kuhamasisha utoaji huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi wenye uhitaji.

“Pamoja na kuwezesha maadhimisho ya mwaka huu visiwani Zanzibar, LSF kupitia uwezeshaji wa kisheria tumekuwa tukifanya kazi ya kukuza upatikanaji wa haki kwa wananchi wote,” amesema Ng’wanakilala.

Mtendaji huyo wa LSF amesema “hasa wanawake kwa kutoa ruzuku, katika mashirika takribani 200 yanayotoa huduma za msaada wa kisheria na wasaidizi wa kisheria zaidi nchi nzima.”

Ng’wanakilala amesema, LSF kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Denmark (DANIDA), pamoja na Jumuiya ya Umoja wa Nchi za Ulaya (EU), limetoa Sh. 27 milioni , kwa ajili ya kufadhili maadhimisho ya wiki ya sheria, visiwani Zanzibar 2021.

Ng’wanakilala amesema, kundi la wanawake linaongoza kwa kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia na kwamba ripoti ya utafiti ya LSF kwa 2020, inaonesha katika kila matukio manne yaliyowasilishwa na wanawake, yalihusiana na ukatili wa kijinsia.

“Hii inaonyesha iko haja ya kuendelea kutoa elimu kwa jamii, kulinda na kutetea haki za makundi mbalimbali hususani wanawake na tunaamini wiki hii itatoa fursa kwa wananchi wa Zanzibar, kupata huduma za msaada ya kisheria pamoja na elimu itakayochochea upatikanaji wa haki,” amesema Ng’wanakilala.

error: Content is protected !!