MWENYEKITI wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini Tanzania, John Shibuda, amesema, kuna ombwe la makada wa kuendeleza siasa za utaifa na uzalendo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Shibuda ametoa kauli hiyo leo Jumatatu tarehe 26 Aprili 2021, wakati akichangia katika Kongamano la Maahimisho ya Miaka 57 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, jijini Dodoma.
Mwanasiasa huyo mkongwe nchini Tanzania, amesema ombwe hilo limesababishwa na marais waliopita, Rais wa Awamu ya Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi, Hayati Benjamin Mkapa (Awamu ya Tatu), Dk. Jakaya Kikwete (Awamu ya Nne) na Hayati Dk. John Magufuli (Awamu ya Tano), kutoandaa makada hao.
“Mimi ni Mwenyekiti wa Baraza la Vyama ya Siasa Tanzania, nasikitika kusema Tanzania ina ombwela sintofahamu la miaka 35.”
“Mzee Mwinyi hakuandaa makada wa kuendeleza maana ya siasa za utaifa na uzalendo. Mzee Mkapa hakufanya hivyo, Dk. Kikwete hakutekeleza hilo, hayati Magufuli hakufanya hilo. Sijui Awamu ya Sita,” amesema Shibuda.
Awamu ya sita, inaongea na Rais Samia Suluhu Hassan.
Kuhusu maadhimisho ya muungano huo, Shibuda ameishauri Wizara ya Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira, ijipange katika kuhakikisha vitabu vilivyoandikwa historia ya muungano inawafikia Watanzania wote, hasa waliozaliwa baada ya muungano huo.
“Mfano leo tuna wanafunzi wasiopungua 200 hapa (kwenye kongamano), ukiwauliza nini maana ya tunu ya muungano na kwa nini muungano ni tunu ya taifa, utapata majibu 200 tofauti, lakini ukimkuta shia au suni ukimuuliza kuhusu mtume Mohamed (S.A.W), makutano yao yako kwenye Msahafu.
“Wakristo makutano ya madhehebu yote yako katika kitabu kitakatifu cha Bibilia, Watanzania wa mfumo wa vyama vingi wa makundi ya wanaharakati mbalimbali hivi makutano yetu ni kwenye kitu gani?” amesema.
Leave a comment