August 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Shaka atembelea MwanaHALISI, Raia Mwema

Shaka Hamdu Shaka, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmsshauri Kuu ya CCM Taifa akiwa katika ofisi za gazeti la MwanaHALISI na Raia Mwema

Spread the love

 

KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ametembelea ofisi za magazeti ya Raia Mwema na MwanaHALISI, ikiwa ni muendelezo wa ziara zake za kutembelea vyombo vya habari, kwa ajili kuimarisha mahusiano kati ya chama hicho na tasnia ya habari nchini. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Shaka ametembelea ofisi hizo zilizoko Kinondoni, jijini Dar es Salaam, leo Jumanne, tarehe 5 Julai 2022, na kupokelewa na viongozi wa kampuni hiyo ambapo amepata fursa ya kufanya mahojiano na waandishi wa magazeti hayo.

Mwanasiasa huyo alishukuru uongozi wa magazeti hayo kwa kumkaribisha”na mimi nishukuru kwa kunikaribisha na nadhani tumepata muda mzuri kubadilishana mawazo na viongozi. Na niko tayari kwa jukumu hili.”

Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Raia Mwema, Joseph Kulangwa, amuelezea Shaka namna gazeti hilo linavyofanya kazi ambapo amesema waandishi wake hawana itikadi za kisiasa badala yake wanafanya kazi ya kuhudumia taifa.

Amesema, kwa sasa gazeti hilo linatoka mara tano kwa wiki na kwamba hivi karibuni litakuwa linatoka kila siku.

Shaka Hamdu Shaka, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmsshauri Kuu ya CCM Taifa akisaini kitabu cha wageni

“Umekuwa kiongozi wa kwanza kitaifa kututembelewa licha ya ahadi zilizokuwa nyuma, tumeamua kukusilikiza ili tujue umekuja na nini na unatufahamu kivipi. Sisi hapa hatuna itikadi, sisi ni Watanzania itikadi ziko nyumbani, tunapokuja hapa tunafanya kazi kuhudumia taifa letu,” amesema Kulangwa na kuongeza:

“Siku zote tunapokutana hapa tunapangiana majukumu, ikiwemo kwenda kwenye vyama kuangalia wanafanya nini, mama yetu (Rais Samia Suluhu Hassan) anafanya nini na wananchi wanafanya nini, kisha tunaangalia uzito wa habari na maslahi yake. Kwa kifupi ndiyo hayo tunafanya kila siku.”

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Hali Halisi Publishers inayochapisha magazeti ya MwanaHALISI, Mawio na Mseto pamoja na gazeti mtandao la MwanaHALISI Online, Saed Kubenea, ameeleza utendaji kazi wa magazeti hayo.

“Magazeti yetu tuko karibu miaka 17 sasa, tulianzia hapa hapa Raia Mwema walianza kwingine wakahama wakaja hapa. Na lengo ni kuunganisha gazeti na MwanaHALISI Online ili utakapokuwepo hapa mfano utakuwa na video, tutapandisha Youtube, ikishapanda Youtube waandishi wataandika habari watapandisha MwanaHALISI Online,” amesema Kubenea na kuongeza:

“Lakini pia itapanda Facebook na Twitter, jioni wanaiboresha inakwenda kwenye gazeti na kesho yake ile habari inapanda kwenye mitandao ya kijamii. Ukikaa hapa unaweza ukasikika Kigoma, Mafia, Mpanda, Mtwara na nje ya mipaka yetu hata Ulaya tunaenda sababu tuna Youtube.”

Kwa upande wake Mkurugenzi Mwenza wa Kampuni ya Raia Mwema, Mbaraka Islam, amesema kitendo cha Shaka kutembelea ofisi za magazeti hayo, kinaashiria kwamba CCM kinatambua umuhimu wa vyombo vya habari.

“Ni jambo la fahari kutemblewa na kiongozi mkubwa wa chama tawala, tunashukuru kwa ujio wako kwa kutambua umuhimu wa vyombo vya habari,” amesema Islam na kuongeza:

“ Tulidhani unatembelea vyombo vya Serikali na chama lakini kutembelea vyombo binafsi maana yake CCM mmeridhia na mko tayari kushirikiana kwa vitendo na si maneno. Na tuko tayari kuilinda tasnia ya habari na kuilinda nchi.”

error: Content is protected !!