August 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

NMB yatoa mikopo ya bilioni 752.7 kwa wajasiriamali wadogo na wa kati

Spread the love

BENKI ya NMB nchini Tanzania imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kuwawezesha wanawake wajasiriamali kote nchini ikiwa ni sehemu ya dhamira yake ya kuhakikisha wanawake wanapiga hatua kiuchumi. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Benki hiyo kati ya Julai 2021 hadi Juni 2022 ilitoa mikopo 37,501 kwa wajasiriamali Wadogo na wa Kati (SMEs) yenye thamani ya bilionin 752.7- huku idadi kubwa ikilenga wafanyabiashara wadogo na wa kati wanawake kwa mujibu wa Afisa Mkuu Huduma Shirikishi wa Benki ya NMB Nenyuata Mejooli.

Mkuu wa Huduma Shirikishi wa Benki ya NMB, Nenyuata Mejooli (katikati) , Mwenyekiti wa Chama cha Wanawake wafanyabiashara Tanzania , Mercy Silla (kulia) na Makamu Mwenyekiti, Rose Romanus (kushoto) wakifurahia baada ya kuzindua Siku ya NMB iliyoadhimishwa na Chama Cha wafanyabiashara wanawake Tanzania kwenye maonyesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanayoendelea.

Akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya NMB, hafla iliyoandaliwa na benki hiyo kwenye banda la Chama cha Wanawake Wafanyabiashara (TWCC) kwenye Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) maarufu sabsaba yanayoendelea kwa ajili ya kuwakumbuka wanawake wajasiriamali, Mejooli alisema benki yake imeweza kubuni bidha mbali mbali ikiwa ni mkakati mahususi wa uwezeshaji wanawake na kuongeza kuwa tangu mwaka 2000, benki imekuwa ikitoa mikopo midogo kuanzia shilingi laki 5 hadi milioni 75.

Alisema kutokana na dhamira ya  benki yake, NMB awali mwaka huu iliorodhesha hati iliyopewa jina la NMB Jasiri Bond katika soko la hisa la Dar es Salaam ambayo ilikusanya bilioni 74.2 ikilenga biashara zinazomilikiwa na wanawake.

 

“Fedha zilizopatikana zitatumika kusaidia biashara zinazomilikiwa na wanawake au wafanyabiashara ambao mnyororo wao wa thamani unanufaisha wanawake wengi. Natoa wito kwa wanawake wajasiriamali kuchangamkia fursa tunapoanza kutoa mikopo,” alisema.

Aliongeza benki yake tayari imetoa bilioni 95.1-katika miaka mitatu iliyopita kama sehemu ya juhudi zake za kusaidia ukuaji wa biashara zinazomilikiwa na wanawake kote nchini.

“Kama benki, tunaelewa kuwa bado kuna idadi kubwa ya watu ambao hawapo kwenye mfumo rasmi wa kifedha ndiyo maana tukaja na kampeni yetu ya malipo ya kidijitali inayoitwa “Teleza Kidigitali inayolenga kuongeza ushirikishwaji wa fedha kupitia bidhaa kama vile NMB MshikoFasta, NMB Pesa Wakala na Lipa Mkononi. Tutaendelea kuwekeza katika utafiti ili kubuni bidhaa nyingi zaidi za kifedha ili kupunguza gepu ya watu ambao hawapo kwenye mfumo rasmi,” alisema.

Mwenyekiti wa Bodi ya Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), Mercy Silla wakati wa hafla hiyo aliishukuru benki hiyo kwa kuendelea kusaidia kuwawezesha wanawake wajasiriamali na kuongeza kuwa chama chake kitaendelea kushirikiana na kusaidia wanawake katika ngazi za chini

Alibainisha kuwa wanawake bado wana fursa nyingi hukuakibainisha kuwa asilimia 30 ya bajeti ya manunuzi imetengwa kwa ajili ya wanawake ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha ushiriki wa wanawake katika mchakato wa manunuzi na kuwataka wanawake kushiriki kikamilifu katika mchakato wa zabuni na kutumia fursa za manunuzi katika miradi mbalimbali.

“Kuna fursa zimewekwa kwa wanawake katika mchakato wa zabuni na manunuzi lakini kwa bahati mbaya wanawake hawajaweza kushiriki kikamilifu na kunyakua fursa kama hizo. Wanawake wanahitaji kutumia fursa hizi zote kikamilifu. Kama chama, tutaendelea kuhamasisha wanawake kuhusu jinsi ya kunyakua fursa kama hizo kuanzia ngazi ya chini,” alisema.

Mkuu wa Huduma Shirikishi wa Benki ya NMB, Nenyuata Mejooli akizungumza wakati kuadhimisha Siku ya NMB kwenye maonyesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba)

Maadhimisho ya Siku ya NMB yalifanyika chini ya kaulimbiu ya “Kuwawezesha Wanawake katika Biashara” yamewakutanisha wanawake kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Simiyu, Tanga, Mara, Njombe, Mwanza kutoka  sekta ya usindikaji wa vyakula, nguo, ngozi, vipodozi, afya na kazi za mikono.

error: Content is protected !!