May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali ya Tanzania yasimamisha gazeti la Uhuru siku 14 p

Gerson Msigwa, Mkuu wa Idara ya Habari na Maelezo

Spread the love

 

SERIKALI ya Tanzania imetangaza kusitisha leseni ya uchapishaji na usambazaji wa Gazeti la kila siku la Uhuru kuanzia kesho Alhamisi tarehe 12 Agosti, 2021. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Ni baada ya gazeti hilo, mali ya chama tawala nchini humo- Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuandika habari ya kupotosha juu ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwa hatongombea katika uchaguzi mkuu ujao 2025.

Katika habari hiyo kubwa kwenye gazeti la leo Jumatano, tarehe 11 Agosti 2021, yenye kichwa cha habari ‘Sina wazo kuwania urais 2025 – Samia’ imeelezwa kunukuliwa katika mahojiano baina ya Rais Samia na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), yaliyorushwa hewani Jumatatu tarehe 9 Agosti 2021.

Mahojiano hayo yalifanyikia Ikulu ya Dar es Salaam.

Taarifa ya Gerson Msigwa, Mkurugenzi wa Idara ya Habari-Maelezo imesema “Ofisi ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari-Maelezo, imebaini habari hiyo ina upungufu wa kisheria na weledi wa taaluma ya uandishi wa habari.”

“…kwa kutoa taarifa za uongo dhidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, kinyume na kifungu cha 50(1)(a),(b), na (d) na kifungu cha 52(d) na (e) vya Sheria ya Huduma za Habari Na.12 ya 2016.”

Msigwa amesema “Rais Samia Suluhu Hassan hajatoa matamshi yoyote ambayo yanaeleza kutokuwa na wazo la kuwania urais mwaka 2025.”

Pia, amesema kwa mujibu wa kifungu cha 10(1) cha Sheria ya Huduma za Habari Na.12 ya 2016, ikiwa gazeti la Uhuru halitaridhika na uamuzi wa Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Habari linayo haki ya kukata rufaa kwa waziri mwenye dhamana ya Habari.

Msigwa amesema, ofisi ya idara ya huduma za habari inaamini adhabu hii itatoa nafasi ya kuboresha masuala yanayohusu weledi wa uandishi wa habari na utekelezaji wa masuala yote yanayohusu uzingatiaji wa Sheria, maadili na kanuni kwa gazeti hilo.

Mkurugenzi huyo amesema, vyombo vya habari vyote “mnakumbushwa kuzingatia Sheria, maadili, kanuni na miongozo mbalimbali inayohusu tasnia ya habari, ili kulinda taaluma na kuleta ustawi wa jamii.”

Msigwa ametangaza uamuzi huo ikiwa tayari Bodi ya Uhuru Media Group (UMG) umewasimamisha Mkurugenzi Mtendaji, Ernest Sungura, Mhariri Mtendaji, Athuman Mbutuku na Rashid Zahoro, msimamizi wa gazeti kutokana na kadhia hiyo.

Uamuzi huo umetangazwa mbele ya waandishi wa habari alasiri ya leo Jumatano, ofisi ndogo za CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wake, Daniel Chongolo.

Aidha, Chongolo aliwaeleza waandishi wa habari kwamba, kwa mamlaka aliyonayo amesimamisha uzalishaji wa gazeti hilo kwa siku saba na uchunguzi zaidi unaendelea kufanywa na kamati iliyoundwa na bodi ya UMG.

error: Content is protected !!