SERIKALI ya Tanzania, imesema imefanikiwa kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa virusi vya Murburg, huku ikiahidi kuutokomeza kwa kufuata miongozo ya Shirika la Afya Duniani (WHO). Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
Taarifa hiyo imetolewa leo Jumanne tarehe 4 Aprili 2023 na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, akizungumzia mwenendo wa ugonjwa huo ulioibuka Machi mwaka huu, wilayani Bukoba, Mkoa wa Kagera.
“Napenda kusema kwamba, mlipuko huu ambao umeathiri sehemu ndogo ya Kagera, tunategemea kwamba tutaumaliza ndani ya siku chache kwa kuzingatia miongozo ya WHO,” amesema Mwalimu.
Mwalimu amesema, tangu ugonjwa huo uibuke hadi sasa, hakuna visa wala vifo vipya vilivyoripotiwa na kwamba idadi ya walioambukizwa imebaki kuwa nane ambapo kati yao, watano wamefariki dunia.
Waziri huyo wa afya amesema, mtu mmoja kati ya watatu waliolazwa kwa matibabu ya ugonjwa huo, ameruhusiwa huku akiitaka jamii inayomzunguka kutombagua kwa kuwa vipimo vimeonyesha hana virusi hivyo.
Amesema wagonjwa wawili wanaendelea na matibabu na kwamba hali zao kiafya zinazidi kuimarika.
Akizungumzia namna mwenendo wa ugonjwa huo ulivyodhibitiwa, Mwalimu amesema wizara yake kwa kushirikinaa na mamlaka mbalimbali nchini, ilifanikiwa kufuatilia watu 212 waliosaidika kukutana na waathirika ambapo watu 35 waliotangana nao moja kwa moja wamemaliza siku 21 za uangalizi na kubainika kwamba hawana dalili za ugonjwa huo.
Amesema, watu hao 35 wameruhusiwa kutoka katika karantini na kurejea katika familia zao.
Leave a comment