SERIKALI imeamua kufufua mradi wa kilimo cha umwagiliaji katika Bonde la Bwigema, Musoma Vijijini mkoani Mara, ulioasisiwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, kisha kukwama 1974. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mara … (endelea).
Taarifa hiyo imetolewa na Ofisi ya Mbunge wa Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo, jana Jumapili, baada ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, kutoa tenda ya upembuzi yakinifu kuhusu mradi huo kwa Kampuni ya Ms Mhandisi Consultancy LTD.
Ofisi hiyo imesema kuwa, utekelezaji wa mradi umekuja baada ya Prof. Muhongo, kumuomba Rais Samia Suluhu Hassan, kuufufua ili kusaidia shughuli za kilimo na ufugaji zinazofanywa na wananchi.
“Rais Samia amepokea na kukubali ombi la kufufua kilimo cha umwagiliaji kwenye Bonde la Bugwema. Serikali iliyoongozwa na Mwalimu Nyerere ilianza kujenga miundombinu ya umwagiliaji kwenye bonde hilo 1974, mradi ukasimama na sasa unafufuliwa,” imesema taarifa hiyo.
Akizungumza na wananchi kuhusu mradi huo, Prof. Muhongo amewataka washirikiane na Serikali katika utekelezaji wake ili ukamilike, huku akiwataka kuwapuuza watu wanaodai kwamba watahamishwa ili kuupisha.
“Serikali imeombwa kuwekeza Bonde la Bugwema na hii inataka iwe na utulivu hakuna atakayehamishwa. Kuna wajanja wanasema mtahamishwa, hamtahamishwa, waruhusu watalaamu wafanye tathimini ili baadae Serikali ipate miundombinu,” alisema Prof. Muhongo.
Kwa upande wa wananchi, wameishukuru Serikali kwa kuukumbuka mradi huo, wakisema ukikamilika utasaidia kuondoa changamoto ya ukame na kuwasaidia kulima kilimo cha biashara katika misimu yote.
Bonde la Bugwema lenye ukubwa wa hekta 10,000, linahudumia vijiji vitatu katika Jimbo la Musoma Vijijini, ikiwemo cha Masinono na Muhoji. Mazao yanayolimwa katika bonde hilo ni mpunga, mahindi, alizeti, dengu na pamba.
Leave a comment