October 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Sakata la Membe, Kinana, Makamba: CCM yaapa kufukuza mwenye kiburi

Spread the love

CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimeweka wazi kwamba, kitamfukuza uanachama mtu atakayeonyesha kiburi dhidi ya sheria, misingi na kanuni za chama hicho. Anaripoti Mwandishi Wetu, Morogoro … (endelea).

Msimamo huo umetolewa leo tarehe 15 Februari 2020, na Dk. Bashiru Ally, Katibu Mkuu wa CCM wakati akizungumza na wanachama wa chama hicho, mkoani Morogoro.

Dk. Bashiru ameweka bayana kuwa, MwanaCCM atakayeonyesha kiburi na jeuri wakati akihojiwa kuhusu tuhuma zinazomkabili za kuvunja misingi ya chama hicho, atafukuzwa uanachama.

“Chama hiki hakina mwenyewe, kama tungekuwa tunatafuta wenye chama tungesema ni cha Mwalimu Nyerere, hayupo ametangulia, tuliobaki ni nani? Ukienda kinyume na misingi ya Mwalimu Nyerere tutakuita kwenye kikao tukuulize kulikoni?  Ukijieleza vizuri tutakubalina namna ya kukusahihisha, ukiwa jeuri na kiburi tutakufukuza,” amesema Dk. Bashiru.

Katibu mkuu huyo wa CCM  amesema hatosita kusaini barua ya kufukuzwa mwanachama wa chama hicho.

“Ndiyo maana tunapoadhibiana kuna wakati wakusameheana, tangu Rais John Magufuli amefika amesamehe watu zaidi 30 waliowahi kufukuzwa, na mimi sijawahi saini barua ya kufukuza. Lakini mkono huu hauogopi kusaini barua ya kufukuza, nimesaini za kusamehe, baada ya vikao kuridhika. Vikao vikiridhika nisaini za kufukuza, nitasaini za kufukuza,” amesisitiza Dk. Bashiru.

Dk. Bashiru ameeleza kuwa, hakuna mtu aliye juu ya sheria za CCM, hivyo hakuna genge la watu watakaotumia fedha zao kukiteka chama hicho.

“Mabalozi hakikisheni chama hakitekwi na kundi la mtu yoyote, pesa zako ni pesa zako, elimu yako ni yako. Hakuna mwenye chama na hakuna aliye juu ya sheria na kanuni za chama. Wote hata mimi nikijisiahau mabega yakapanda kama mwendawazimu nitashughulikiwa,” amesema Dk. Bashiru na kuongeza:

“Siwezi  nikatisha wanachama sababu wengine wananiita baba lao, mimi siyo baba lao, nikikosea nashughulikiwa. Hizo baba lao ni nyimbo za sifa na ukilewa sifa unaweza kujisahahu, chama hiki siyo cha Rais Magufuli, Rais Shein ni cha wananchi wote.”

Msimamo huo wa Dk. Bashiru umekuja ikiwa zimesalia siku nne, kwa Kamati Ndogo ya Udhibiti na Nidhamu ya CCM kuwasilisha taarifa ya mahojiano ya Bernard Membe, Waziri wa Mambo ya Nje Mstaafu na Makatibu Wakuu Wastaafu wa chama hicho, Mzee Yusuph Makamba na Abdulrahman Kinana, katika vikao husika.

Mnamo tarehe 12 Februari mwaka huu, Kamati Kuu ya CCM ilitoa agizo kwa kamati hiyo kuwasilisha taarifa ya mahojiano ya wanachama hao katika vikao husika, ndani ya siku saba.

Membe, Mzee Makamba na Kinana walihojiwa katika nyakati tofauti hivi karibuni na Kamati Ndogo ya Udhibiti na Nidhamu ya CCM, ili kujibu tuhuma zinazowakabili za kukiuka maadili ya chama hicho.

error: Content is protected !!