October 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mwambe aitosa Chadema, amkaanga Mbowe

Cecil Mwambe, aliyekuwa Mbunge wa Ndanda kwa tiketi ya Chadema

Spread the love

CECIL Mwambe, Mbunge wa Jimbo la Ndanda, amejiuzulu wadhifa huo baada ya kukihama chama chake cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), na kurejea katika Chama cha Mapinduzi (CCM). Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea).

Mwambe ametangaza uamuzi huo leo tarehe 15 Februari 2020, mbele ya Humphrey Polepole, Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, katika ofisi ndogo za chama hicho zilizoko Mtaa wa Lumumba, jijini Dar es Salaam.

“Mimi Cecil David Mwambe, najivua uanachama wangu wa Chadema pamoja na nafasi zangu nilizokuwa nazo ndani ya chama. Ikiwa pamoja na ubunge kuwawakilisha wananchi wa Ndanda,” ameeleza Mwambe.

Mwambe ameeleza kuwa, hatua yake ya kuhamia CCM haijatokana na shinikizo kutoka kwa mtu yeyote, bali imetokana na hiari yake mwenyewe.

“Ninafahamu niliposhinda Ubunge wa Jimbo la Ndanda mwaka 2015, ushindi wangu ulitokana na wapiga kura na wakazi wa Jimbo la Ndanda. Hata hivyo, leo hii kwa hiari yangu mwenyewe kwa kutumia haki yangu kikatiba, nimeamua kujiunga na CCM,” amesema Mwambe.

Kuhusu hatma ya wapiga kura wake wa Jimbo la Ndanda, Mwambe amesema atagombea tena jimbo hilo kupitia CCM, katika Uchaguzi Mkuu wa Mwezi Oktoba 2020.

“Nitagombea tena ubunge katika uchaguzi ujao, kupitia  chama bora ambacho kinaheshimu demokrasia ya ndani, kina misingi imara ya uongozi, kinaheshimu wanachama na viongozi wake. Na kinajali maadili ya wanachama na viongozi wake na nitawaomba wananchi wangu wawe na subira na wanipokee endapo nitapewa ridhaa ya kufanya ivyo,” amesema Mwambe:

“Nataka tu niwakumbushe kwamba, ushindi wangu wa ubunge mwaka 2015 ulitokana na wakazi wa Jimbo la ndanda, ambao waliniamini, na bado ninaamini bado wapo na wako tayari kuhakikisha Chama Cha Mapinduzi kinashinda.”

Licha ya kukiri kwamba amerejea CCM kwa hiari yake mwenyewe, Mwambe amesema changamoto alizokumbana nazo ndani ya Chadema, ndizo zilizomsukuma kuchukua hatua hiyo.

“Nimekutana na changamoto kadha wa kadha ndani ya chama hiki kinachojinasibisha kwa umma kuwa ni chama cha demokrasia lakini ukweli ni kwamba demokrasia hii inayoimbwa majukwaani haipo ndani ya Chama kama watu wanavyodhani.

Inazungumzwa tu mdomoni kuwahadaa wananchi lakini kiuhalisia na katika matendo demokrasia hiyo haipo,” amesema Mwambe.

Mwambe amedai kuwa, alianza kubaini kwamba Chadema haina demokrasia, pindi alipotangaza kugombea uenyekiti wa chama hicho, ambapo alianza kuundiwa zengwe.

“Kama mnakumbuka wakati wa mchakato wa uchaguzi wa Chadema kuanzia ngazi ya kanda hadi uchaguzi mkuu, figisu nyingi sana zilitokea hasa kwa wagombea ambao tulionekana tuna nguvu na uwezo wa kushinda, lakini hatukuwa wapenzi wa bwana mkubwa na kila mmoja alishuhudia jinsi mimi mwenyewe nilivyokuwa natendewa,” amesema Mwambe.

Mwambe amesema “Licha ya kupewa fomu za kugombea uenyekiti wa Chadema taifa na kubainisha mambo ambayo ningekwenda kuyafanya iwapo ningechaguliwa, lakini nia yangu hiyo ya kidemokrasia iligeuka kuwa shubiri na silaha ya kushambuliwa kwangu na watu waliokuwa wanatumwa na washindani wangu katika nafasi hiyo ndani ya  Chadema.”

error: Content is protected !!