February 28, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Sakata la Korosho: Mbunge ajiweka rehani

Zao la Korosho

Spread the love

MBUNGE wa Nchinga kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Hamidu Hassan Bobali, ameituhumu serikali kudhulumu wakulima wa korosho katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Pwani. Anaripoti Mwandishi Wetu kutoka Dodoma … (endelea).

Akizungumza bungeni mjini Dodoma wakati wa kuchangia taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma, Bobali alisema, serikali imeuza tani laki moja za korosho kwa Sh. 4,180 kwa kila kilo, lakini yenyewe imewalipa wakulima Sh. 2,600 kwa kilo.

“Serikali imekuja kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo na kusema, gharama za kununua korosho kwa kila kilo, ni Sh. 3,8000 (elfu tatu na mia nane). Lakini yenyewe imeuza kila kilo moja ya zao hilo, kwa Sh. 4,180. Hivyo tunataka tuelezwe hii chenji yetu itarudi ama tumeingizwa tena mkenge,” alihoji Bobale.

Aliongeza, “…huu ni wizi wa wazi kabisa. Hatuwezi kukubali wananchi wapunjwe stahiki zao. Haiwezekani. Tunataka wakulima hawa walipwe kama ambavyo Rais John Pombe Magufuli aliahidi na aliutangazia ulimwengu.”

Kauli hiyo ya Bobali ilizua tafrani kubwa kutokana na baadhi ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na baadhi ya mawaziri kupinga taarifa kuwa wakulima wanalipwa kiasi cha Sh. 2,600 kwa kila kilo ya korosho.

Bobali alidai kuwa kitendo cha serikali kununua korosho kwa wakulima moja kwa moja na kisha kuziuza, hakina tofauti na kile kinachofanywa na wanunuzi wadogo, maarufu kama Kangomba.

Akahoji, “hivi hapa kuna tofauti gani kati ya serikali na kile kinachofanywa na Kangomba? Mbona hapa nayo imekuwa Kangomba?”

Kufuatia mzozo huo, ndipo Bobali akanyanyuka na kusema, “ikiwa atatokea mbunge anayeweza kuthibitisha kuwa nimesema uongo. Kwamba, wakulima hawalipwi Sh. 2,600 kwa kila kilo ya korosho. Kwamba wanalipwa kiasi tofauti na hiki nilichokitaja, basi niko tayari kujiuzulu ubunge wangu.”

Akiongea kwa kujiamini, Bobali alisema, “sikuja hapa kufanya siasa. Nimeletwa hapa na wananchi wa Nchinga na watanzania wengine kwa ujumla, kutetea maslahi yao. Ninachokisema nina uhakika nacho.”

Mara baada ya kauli hiyo, hakuna mbunge yeyote aliyejitokeza tena kumpinga mbunge huyo.

error: Content is protected !!