May 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Saa 48 za mwili wa Magufuli Chato

Spread the love

 

WANANCHI wa Chato, mkoani Geita leo Alhamisi tarehe 25 Machi 2021, watauaga mwili wa mpendwa wao, Dk. John Pombe Joseph Magufuli. Anaripoti Mwandishi Wetu, Chato … (endelea).

Mwili wa Dk. Magufuli, ulianza kuagwa Dar es Salaam, Dodoma, Zanzibar na Mwanza, jana jioni Jumatano, uliwasili nyumbani kwao, Chato kwa ajili ya maziko, yatakayofanyika kesho Ijumaa.

Dk. Magufuli, ni mzaliwa wa Chato tarehe 29 Oktoba 1959, ambapo aliongoza jimbo hilo akiwa mbunge, kwa miaka 20 kuanzia mwaka 1995 hadi 2015, alipogombea urais na kushinda.

Shughuli hiyo ya kuaga mwili wa Dk. Magufuli, aliyefariki dunia tarehe 17 Machi 2021, Hospitali ya Mzena, Makumbusho mkoani Dar es Salaam, itafanyika kwa siku mbili sawa na saa 48 katika Uwanja wa Magufuli, Chato.

Maelfu ya wakazi wa Chato na wageni mbalimbali; mawaziri, wabunge, wakuu wa taasisi, wanasiasa, wamefurika uwanjani hapo wakiongozwa na Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa.

Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama akiwemo, Mkuu wa Majeshi, Jenerali Venance Mabeyo ni miongoni mwa waliojitokeza uwanjani hapo, kumuaga aliyekuwa Amiri Jeshi Mkuu.

Wengine ni; Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, ambaye atawaongoza wana Chato kutoa heshima za mwisho. Pia, Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Bashiru Ally nao wamekwisha.

Waombolezaji, watauaga mwili huo hadi saa 12:00 jioni ya leo Alhamisi, kisha mwili huo utarudishwa nyumbani ambapo maombolezo ya kifamilia yataendelea.

Kesho Ijumaa, ratiba itaanza asubuhi kwa mwili wa Dk. Magufuli kupelekwa kanisani Katoliki Chato, ambalo alibatishwa na kuwa na utaratibu wa kusali kila alipokwenda mapumziko, itafanyika ibada fupi itakayoongozwa na Paroko, Sosper Tibaijuka.

Baada ya Ibada kumalizika, familia itatoa heshima za mwisho kisha utapelekwa Uwanja wa Magufuli ambapo napo kutafanyika Misa Takatifu, itakayoongozwa na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Gervas Nyaisonga.

Shughuli hiyo ya mwisho hapa duniani ya Dk. Magufuli, itaongozwa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ambaye kwa mujibu wa ratiba inaonyesha atazungumza.

Wengine watakaozungumza ni pamoja na marais wastaafu wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete na Al Hassan Mwinyi.

Baada ya shughuli hiyo kumazilika uwanjani hapo, mwili wa Dk. Magufuli utakwenda eneo la mazishi ambapo, ibada ya mazishi itafanywa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge-Ngara, Severine Niwemugizi.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI TV na MwanaHALISI Online kwa habari na taarifa mbalimbali

error: Content is protected !!