May 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Chato walivyoupokea mwili wa Magufuli, kulazwa kwake

Spread the love

 

MWILI wa aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, umewasili nyumbani kwao, Chato Mkoa wa Geita ukitokea Mwanza. Anaripoti Mwandishi Wetu, Chato … (endelea).

Msafara huo umewasili Chato Mjini leo Jumatano, tarehe 24 Machi 2021, saa 12:00 jioni, ukitokea Mwanza, ambako maelfu ya wananchi wa mkoa huo na maeneno jirani waliuaga.

Msafara huo, umetumia zaidi ya saa nne, barabarani kwani ulianza Mwanza saa 7 mchana.

Mara baada ya msafara huo kuwasili, ulipitishwa maeneo kadhaa ya mitaa ya Chato, hali iliyosababisha vilio na simanzi kutoka kwa waombolezaji, hususan walipokuwa wakiona gari lililobeba jeneza la mpendwa wao.

Mwili wa Dk. Magufuli, aliyezaliwa Alhamisi ya tarehe 29 Oktoba 1959, umewasili kwao kwa ajili ya kuhifadhiwa kwenye makazi yake ya milele, Ijumaa 26 Machi 2021.

Maelfu ya wananchi wa Chato na maeneo jirani, wameupokea mwili wa mpendwa wao, aliyelitumikia Taifa kwa nafasi ya urais kwa miaka mitano na miezi mitano.

Kabla ya kufika Chato, msafara huo ulipita Busisi- Sengerema- Geita- Katoro- Bwanga kisha Chato ambako kote huko, umati ulikuwa mkubwa.

Dk. Magufuli, amekuwa mbunge wa Chato kwa takribani miaka 20 tangu mwaka 1995 hadi 2015 na baadaye kugombea urais na kushinda.

 

Ulipofika Geita Mjini, wananchi waliusimamisha msafara huo hususan gari lililobeba mwili wa Dk. Magufuli hali iliyokuwa ikiwafanya askari kuwasogeza pembeni.

Baadhi ya wakazi waliozungumza na MwanaHALISI Online wamesema, wamempoteza kiongozi waliokuwa wanampenda.

“Rais wetu wameondoka bado tunampenda. Alikuwa akija mapumziko, sisi wafanyabiashara tulikuwa tunaneemeka na ujio wake, lakini sasa ndio basi,” amesema Mary Masanja.

Wakati ukizungushwa maeneo mbalimbali ya Chato, vilio vilitawala kutoka kwa waombolezaji waliokuwa wamejipanga barabarani kumuaga kisha ukapelekwa, nyumbani kwake.

Mwili wa Dk. Magufuli kesho Alhamisi, utapelekwa uwanja wa mpira ambapo utaagwa kwa siku nzima Ijumaa ya 26 Machi 2021, utazikwa nyumbani hapo.

error: Content is protected !!