Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Z’bar wamtaka Rais Mwinyi aongoze kama Magufuli
Habari za SiasaTangulizi

Z’bar wamtaka Rais Mwinyi aongoze kama Magufuli

Spread the love

 

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesema, vijana wengi visiwani humo, wanataka Serikali ya Rais Hussein Mwinyi, iongoze kama alivyokuwa anaongoza Hayati Rais John Magufuli (61). Anaripoti Mwandishi Wetu, Geita … (endelea).

Abdulla ameyasema hayo leo Alhamisi tarehe 25 Machi 2021, katika shughuli ya kuuaga mwili wa Hayati Rais Magufuli, inayofanyikiwa Uwanja wa Mpira wa Magufuli, Chato mkoani Geita.

Amesema baada ya mwili wa Hayati Rais Magufuli kuagwa visiwani Zanzibar, alianza kupokea salamu nyingi kutoka kwa vijana hao, ambao walimueleza kwamba wanataka kuongozwa kama alivyokuwa anaongoza mwanasiasa huyo.

Hayati Rais Magufuli aliiongoza Tanzania katika Serikali ya awamu ya tano, kwa miaka mitano na miezi mitano mfululizo, kuanzia tarehe 5 Novemba 2015 hadi 17 Machi 2021.

Aliingia madarakani baada ya kushinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na 2020.

“Juzi mwili wa marehemu walipoutembeza Zanzibar, vijana walikuwa wanaufuata mwili kila mahala, wakasema makamo meseji yetu, tunataka tuendelee kuongozwa kama vile alivyokuwa anaongoza Hayati Rais Magufuli, hiyo ndio salamu ya hao vijana, nimekuwa nikipokea salamu nyingi,” amesema Adbdulla.

Jeneza lililobeba mwili wa Hayati Rais Magufuli lilitembezwa visiwani Zanzibar kwa ajili ya wananchi kutoa heshima zao za mwisho, juzi Jumatano tarehe 23 Machi 2021.

Hayati Rais Magufuli alifariki dunia tarehe 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena, Mkaumbusho mkoani Dar es Salaam, alikokuwa anapatiwa matibabu ya matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo.

Akizungumzia uongozi wa Hayati Rais Magufuli, Abdulla amesema amefanikiwa kuliacha Taifa salama, huku likiwa limepiga hatua katika ukuaji uchumi, kutoka uchumi wa chini hadi wa kati.

“Ameliacha taifa hili likiwa salama na amani, tumeona amelitoa kwenye uchumi wa chini kufika wa kati kabla ya muda uliotabiriwa na wataalamu, ni jambo kubwa sana, heshima ya Hayati Rais Magufuli itaendelea kukumbukwa milele na milele,” amesema Abdulla.

Abdulla amesema, Hayati Magufuli ameacha alama kila mahali.

“Sote tumekuwa mashahidi kila kundi ndani ya nchi yetu, kila sekta ndani ya nchi yetu hakuna pahala ambapo marehemu Hayati Rais Magufuli hakuacha alama, iwe kwenye vituo vya afya, shule, kwenye usafiri wa anga,” amesema.

“Mapato kwenye maeneo yote, kila pahala ameacha alama, ni vigumu kujaribu kuyachambua maana hutayamaliza ni marefu sana,” amesema Abdulla.

Makamu huyo wa pili wa Rais Zanzibar, amewaomba viongozi wa serikali na Watanzania kwa ujumla, kumuenzi Hayati Rais Magufuli kwa kupiga vita rushwa na ubadhirifu wa mali za umma.

“Ni wajibu wetu viongozi na Watanzania wote tuungane kwa pamoja kuyaenzi mazuri yote. Tukiendelea kushikama tutapiga hatua kubwa sana, lakini kumuenzi ni kuendelea na sera zake za kuchapa kazi, kuwa waaminifu, kupiga vita ubadhirifu, kuweka mbele uzalendo na utaifa wetu,” amesema Abdulla.

Mwili wa Hayati Rais Magufuli unazikwa kesho Ijumaa tarehe 26 Machi 2021, kijijini kwao Chato mkoani Geita.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

Habari za Siasa

CCM yakemea ufisadi, yaipa kibarua TAKUKURU

Spread the love  CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimekemea vitendo vya ubadhirifu wa...

Habari za Siasa

Bajeti ya Ikulu 2024/25 kuongezeka, bunge laombwa kurudhia Sh. 1.1 trilioni

Spread the love  WIZARA ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa...

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

error: Content is protected !!